Habari MsetoSiasa

Raila atengwa na washirika wake kisiasa kuhusu 2022

October 29th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KUTEULIWA kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa Mjumbe Maalumu wa Muungano wa Afrika (AU), kumefanya waliokuwa washirika wake kwenye uchaguzi mkuu uliopita kumtenga zaidi wakijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Vinara wenzake katika muungano wa NASA, ambao wametangaza kuwa watagombea urais kwenye uchaguzi wa 2022, wanasema kwamba sasa Bw Odinga amepanda hadhi na anafaa kuwaachia nafasi ya kucheza siasa za humu nchini.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wameanza mikakati yao kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 bila Bw Odinga.

Akiongea akiwa Kaunti ya Taita Taveta mwishoni mwa wiki, Bw Musyoka alisema bado ana nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa 2022 bila NASA. Bw Kalonzo alisema kuwa muungano wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga haujaadhiri azimio lake la kugombea urais.

“Safari ya Canaan bado ipo. Wengine walidhani kuwa tunaenda tu kama Nasa,” alisema.

Wabunge wa Wiper waliondamana naye walirejelea mjadala kuhusu mkataba wa NASA kwenye uchaguzi mkuu uliopita wakilaumu chama cha ODM kwa kuupuuza.

“Kulikuwa na makubaliano kuwa Bw Odinga ataunga mkono kiongozi wa chama changu katika uchaguzi wa 2022. La kushangaza ni kuwa wabunge wa ODM wanazunguka wakimpigia debe Bw Odinga),” alisema mbunge wa Wudanyi Dan Mwashako.

Bw Musyoka alisisitiza kuwa jina lake litakuwa kwenye debe liwe liwalo.

Wachanganuzi wanakubaliana na wabunge wa ODM kwamba uteuzi wa Bw Odinga AU hautamzuia kushiriki siasa za humu nchini.

Hata hivyo, wabunge wa Wiper wanasema kwa kuwa Bw Odinga amepata nafasi ya kufanya kazi AU, anafaa kumuunga mkono Bw Musyoka.

Naibu kiongozi wa wachache bungeni Bw Robert Mbui vilevile alisema kuwa chama cha Wiper kitahakikisha kiongozi wao atagombea urais kwenye uchaguzi ujao.

“Ikiwa Bw Kenyatta ni rais wa nchi, Bw Odinga anadaiwa kuwa rais wa wananchi kwa nini tusimfanye Bw Musyoka kuwa rais wa serikali ijayo?” alisema.

Bw Mudavadi na Bw Wetangula wameripotiwa kukamilisha mipango ya kuunganisha vyama vyao vya kisiasa kwa lengo la kubuni chama kimoja kikuu cha jamii ya Waluhya. Kuzinduliwa kwa chama hicho kitakachofahamika kama All Kenyans Alliance Party utakuwa mwisho wao katika NASA.

Muungano wa Waluhya umeshabikiwa hata na wanachama wa ODM eneo la Magharibi huku Gavana wa Kakamega Wycliff Oparanya, ambaye ni naibu wa Bw Odinga akiahidi kujiunga nao ukizinduliwa rasmi.

Ikiwa Bw Mudavadi na Bw Wetangula watazindua muungano wa jamii ya Waluhya na Bw Musyoka agombee urais kivyake anavyodai, Bw Odinga na chama chake cha ODM atalazimika kuweka mikakati mipya iwapo atagombea urais 2022.

Bw Wetangula alijitenga na Bw Odinga wakati ODM kilipompokonya wadhifa wa kiongozi wa wengi katika seneti.

Kufaulu kwa muungano wa jamii ya Waluhya kutampokonya kura nyingi za eneo la Magharibi ambalo Naibu Rais William Ruto pia ameweka mikakati ya kupenya jinsi anavyofanya eneo la Pwani.