Raila atetea kuzungushwa kwa urais

Raila atetea kuzungushwa kwa urais

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amemtetea Rais Uhuru Kenyatta kuhusu matamshi ya kwamba mamlaka ya urais yanafaa kuwa mikononi mwa jamii tofauti na zile mbili ambazo zimeongoza tangu Kenya ilipopata uhuru.

Mnamo Jumamosi, Rais Kenyatta aliashiria kuwa hatamuunga mkono naibu wake, Dkt William Ruto kwa urais 2022 aliposema inafaa uongozi uende kwa jamii tofauti na ya Wakikuyu au Wakalenjin.

Matamshi hayo yaliibua hasira kutoka kwa wafuasi wa Dkt Ruto, ambao walisema Rais anaendeleza ukabila.Bw Odinga akizungumza jana alipokutana na vijana mtaani Karen, Nairobi, alisema Rais Kenyatta hakukosea kwa matamshi hayo kwani Kenya inafaa kufuata mfumo wa mataifa mengine ambapo urais huzungushwa kutoka eneo moja hadi lingine.

“Kenya ni jamii ya makabila mengi, kwa hivyo lazima izingatie kila kabila. Kuna nchi ziko na mfumo wa kuzungusha urais kutoka eneo moja hadi lingine. Nchini Amerika, kama wewe ni rais ni lazima naibu wako awe wa kutoka eneo tofauti. Nchi tofauti hushughulikia suala hilo kwa njia tofauti kwa hivyo si vibaya kujadili jambo hilo,” akasema.

Kulingana naye, athari za urais kuwa mikononi mwa makabila machache kila mara ni kwamba makabila mengine hukosa uwakilishi mwafaka serikalini, na hivyo kusahaulika katika ajira na maendeleo.

“Lazima tushirikishe watu wote serikalini. Ushuru hutozwa kutoka kwa kila mtu kwa hivyo hakufai kuwe na ubaguzi,” akasema.

Hata hivyo, alikemea viongozi wenye malengo ya kuunda vyama vya kimaeneo akisema mwenendo huo utafanya ukabila kukita mizizi nchini.

Katika siku za hivi majuzi, eneo la Pwani limegonga vichwa vya habari kuhusu viongozi wanaojikakamua kuunda chama kimoja cha kutetea masilahi ya Wapwani.

“Tujiepushe na siasa za ukabila. Tusizungumzie kuungana kikabila bali kuungana kama Wakenya na tujadili sera,” akasema.Alirejelea madai yake kuwa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) yatasaidia kukabiliana na umaskini hasa miongoni mwa vijana.

You can share this post!

Mwanamume afa akiramba uroda lojing’i

Maraga awataka majaji kusimama kidete akistaafu