Raila atetea mali fiche ya Uhuru

Raila atetea mali fiche ya Uhuru

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, Jumatano alimtetea vikali Rais Uhuru Kenyatta baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa mabwanyenye walioficha mabilioni ya fedha katika nchi za kigeni.

Rais Kenyatta alitajwa Jumatatu kwenye ufichuzi huo, maarufu kama ‘Pandora Papers’.

Lakini Jumanne, Bw Odinga alimtetea Rais Kenyatta, akisema si kosa kwa Wakenya kuwa na akaunti kama hizo, ikiwa hazitumiwi kuipora nchi au kuhifadhi mali ya wizi.

“Nina imani ukweli kamili utajulikana. Rais amesema atatoa maelezo ya kina kuhusu madai hayo. Ningemtaka kila Mkenya mwenye akaunti hizo kujitokeza na kutangaza wazi,” akasema Bw Odinga, kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya redio zinazotumia lugha ya Kikalenjin.

Kauli yake inajiri huku Rais Kenyatta na jamaa zake wakiendelea kujipata lawamani kuhusiana na sakata hiyo.

Tayari, waandani wa Naibu Rais William Ruto wamemkosoa vikali Rais Kenyatta, wakisema ni kosa kwa kiongozi yeyote aliye mamlakani kuwa na akaunti za siri ughaibuni.

Wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu) na Gladys Shollei (Uasin Gishu) walisema ni makosa kwa kiongozi wa nchi na jamaa zake kuweka kiwango kama hicho cha fedha katika mataifa ya kigeni, ihali zingechangia sana kustawisha uchumi wa Kenya.

“Ikiwa tungejiamini wenyewe na kuwekeza fedha hizo nchini, Wakenya hawangekuwa wakilalamikia ukosefu wa ajira. Tunaweza kushughulikia changamoto zinazotukumba kama vile deni kubwa la taifa, ikiwa fedha hizo zinaweza kurejeshwa nchini,” akasema Bw Ichung’wa, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Bi Shollei alisema: “Ikiwa viongozi waliopo nchini ni wazalendo, basi wanapaswa kuwekeza fedha zao nchini Kenya.”

Mashirika ya kutetea haki za umma pia yamejitokeza vikali yakiitaka taasisi za kukabiliana na wizi wa fedha za umma kama vile Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kuchunguza ikiwa kuna uwezekano Rais Kenyatta amekuwa akitumia ushawishi wake kuifaidi familia yake kifedha.

“Ikizingatiwa tumeshuhudia sakata za awali, ambapo watu maarufu wamenaswa kwa kutumia akaunti za siri kuipora nchi, madai hayo yanapaswa kuchunguzwa kikamilifu,” akasema Bw Ndung’u Wainaina, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa kuhusu Mizozo na Sera (ICPC).

Shinikizo hizo zinajiri huku Mahakama ya Juu ikitarajiwa kuandaa kikao kuamua ikiwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Chris Okemo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Umeme Kenya (KP), Samuel Gichuru, watasafirishwa Uingereza kusikiliza mashtaka dhidi yao kuhusu ulanguzi wa fedha.

Kwenye kikao hicho kilichopangiwa kufanyika leo, majaji wataamua kuhusu ni nani kati ya Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki, na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Hajji, anayepaswa kutoa kibali kwa wawili hao kusafirishwa Uingereza.

Wawili hao wanadaiwa kufungua kampuni za siri ughaibuni walizotumia kuficha fedha walizopora humu nchini.

Kijumla, wanadaiwa kuipora nchi zaidi ya Sh900 milioni.

Licha ya agizo la kukamatwa kwao kutolewa karibu miaka kumi iliyopita na mamlaka za Uingereza, wamekuwa wakitumia mahakama mbalimbali nchini kukwepa kukamatwa.

Hii si mara ya kwanza kwa Wakenya kutajwa kuwa miongoni mwa watu walioficha akaunti za siri katika nchi za kigeni.

Mnamo 2016, Wakenya 191 walitajwa kuficha fedha zao katika akaunti za siri ughaibuni kwenye ufichuzi mwingine, maarufu kama ‘Panama Papers’.

Miongoni mwa waliotajwa kwenye orodha hiyo ni aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu, Kalpana Rawal, wafanyabiashara James Gitau Singh, Feisal Mohammed, Mwendia Nyaga, Aly Popat kati ya wengine.

Wadadisi wa masuala ya uchumi wanasema watu wengi hupendelea kuweka fedha zao katika akaunti hizo ili kukwepa kulipa ushuru katika nchi zao.

You can share this post!

Aliyeshtakiwa kwa kumjeruhi mmiliki wa mkahawa jijini kwa...

Unyakuzi watishia faida za misitu ya Kaya