Raila atetea miradi ya handisheki

Raila atetea miradi ya handisheki

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga amewasuta baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa kuchochea umma kuhusiana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta eneo la Nyanza hivi majuzi ambapo alizindua miradi kadha ya maendeleo.

Kiongozi wa taifa alizindua miradi ya barabara na maji katika kaunti za Kisumu na Siaya. Rais Kenyatta pia aliongoza sherehe za kataifa za Madaraka Dei, kwa mara ya kwanza, mjini Kisumu.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu, Bw Odinga alisema kuzinduliwa kwa miradi hiyo na kuandaliwa kwa sherehe hizo katika eneo hilo la Nyanza hakufai kuchukuliwa kama hatua ya kupendelea eneo hilo, kama baadhi ya wanasiasa walidai.

“Bw Odinga anaamini kuwa enzi za kuchochea jamii moja dhidi ya nyingine zimeisha. Wale wanaotaka kuwarejesha Wakenya katika enzi hizi wanaishi katika nchi nyingine,” ikasema taarifa ya Bw Odinga iliyotumwa kwa vyombo vya habari na msemaji wake Dennis Onyango.

Bw Odinga alisema madai kama hayo zinaenda kinyume cha “moyo wa kujenga Kenya yenye umoja na ufanisi kutokana na makabila na maeneo mengi”. Alisema viongozi wa kisiasa wanafaa kuwa mstari wa mbele kuendeleza umoja na kuwahimiza wafuasi wao kutumia uwezo na rasilimali walizo nazo kwa ajili ya kujiendeleza na kustawisha Kenya.

“Sherehe za Madaraka Dei mnamo Juni 1, na shughuli zilizotangulia zinaenda sambamba na mtindo ulioanzishwa mnamo 2013 wa kutoa nafasi kwa kaunti mbalimbali kuonyesha kile ambacho kila kaunti kinaweza kuchangia, kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa, katika ustawi wa Kenya.”

“Hakuna mradi hata mmoja uliozinduliwa au uliotajwa wakati wa sherehe za Madaraka Dei zinamilikiwa na kaunti ya Kisumu pekee. Hizi ni miradi ya kitaifa ambayo inalenga kufaidi Wakenya wote, husasan wanaotoka ukanda wa magharibi mwa Kenya,” Bw Odinga akaeleza.

Alitoa ufafanuzi huo kujibu wabunge kutoka kaunti za jamii ya Waluhya waliodai kuwa anatumia handisheki kati yake na Rais Kenyatta kuvutia miradi eneo lake la Luo Nyanza na kutenga maeneo yao yalimpa Odinga kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Wabunge; Ayub Savula (Lugari), Didmus Barasa (Kimilili) na Titus Khamala (Lurambi) miongoni mwa wengine walisema Bw Odinga hujali wakati wa magharibi akitaka kura pekee “lakini anapeleka miradi ya maendeleo kwao.”

Mwenzao wa Ikolomani Benard Shinali naye alisema serikali ya Jubilee inafaa kutekeleza miradi ya maendeleo katika eneo la magharibi kwa sababu wakati wa eneo waliipa wabunge wanane katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Lakini Bw Odinga alisema miradi iliyozinduliwa kama vile Bandari ya Kisumu na reli iliyokaribitiwa ya kutoka Naivasha hadi Kisumu itasaidia kaunti nyingi wala sio Kisumu pekee.

  • Tags

You can share this post!

Utangamano wa kitaifa ni moja ya malengo muhimu ya elimu,...

Mwanariadha mkimbizi Mkongo aliyekimbia kutoka Nairobi hadi...