Habari

Raila atetea Mwende Mwinzi

October 5th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amewakosoa wabunge kwa kupinga uteuzi wa Bi Mwende Mwinzi kuwa balozi wa Kenya nchini Korea Kusini akisema Katiba inamruhusu kuhudumu katika wadhifa huo licha ya kuwa na uraia wa mataifa mawili.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari Jumamosi, Bw Odinga alisema Katiba ya sasa iliyozinduliwa 2010 inaruhusu mtu aliye na uraia wa mataifa mawili kufurahia haki zote za raia wa Kenya.

Bi Mwende alizaliwa nchini Amerika na baba Mkenya pamoja na mama Mwamerika.

Bw Odinga anarejelea kipengee cha 14 cha Katiba ya sasa inayosema kuwa mtu aliyezaliwa na Mkenya aliyekuwa akiishi ng’ambo, kabla ya kuzinduliwa kwa Katiba hii, atachukuliwa kuwa raia wa Kenya.

“Kwa hivyo, hatua ya wabunge kukataa uteuzi wa Bi Mwende kuwa balozi wa Kenya haina maana na ni sawa na kumchukulia kama mhalifu ilhali sheria na katiba inamlinda,” akasema Bw Odinga.

“Kwa kupinga uteuzi wa Mwende wabunge pia wanaua moyo na umuhimu wa uraia mbili ambayo kwayo Wakenya waliomba wapewe haki sawa ughaibuni na nyumbani ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa letu,” akaongeza.

Lakini Wabunge kupitia, kamati kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni, wamesisitiza kuwa Bi Mwende anapasa kuasi uraia wa Amerika, alioupata kwa misingi ya kuzaliwa huko, ili aweze kuanza kuhudumu kama balozi wa Kenya nchini Korea Kusini.

Hata hivyo, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kajiado Kusini Katoo Ole Metito, ilimpiga msasa na kuamua kuwa amehitimu kazi hiyo.

“Lakini sharti Bi Mwende abatilishe uraia wake wa Amerika kwanza kabla ya kulishwa kiapo kuanza kazi hii kulingana na hitaji la sheria ya Uongozi na Maadili ya Maafisa wa Serikali,” akasema Bw Metito alipowasilisha ripoti ya kamati hiyo bungeni.