Raila atetea Uhuru kuhusu mapungufu ya Jubilee

Raila atetea Uhuru kuhusu mapungufu ya Jubilee

Na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amemtaka Naibu Rais William Ruto kukoma kumlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa serikali kukosa kutekeleza ahadi mbalimbali kwa wananchi.

Akihutubu jana katika Kaunti ya Vihiga kwenye kikao maalum cha vijana, Bw Odinga alidai Dkt Ruto ndiye anastahili kubeba lawama zote zinazohusiana na utendakazi duni wa utawala wa Jubilee.

Wakati huo huo, alijitenga na kutofanikiwa kwa utendakazi wa serikali ya Jubilee, akisema hakuna kiongozi wa chama chake anayehudumu kama waziri.

“Ruto ndiye alitoa ahadi nyingi za Jubilee ambazo bado hazijatimizwa. Alitwambia kuhusu mpango wa serikali kubuni nafasi milioni moja za kazi na kutengenezwa kwa viwanja vya michezo vya kisasa katika kila kaunti,” akasema Bw Odinga.

Akaongeza: “Vile vile, alitwambia kuhusu mradi wa vipakatalishi ambao haukutekelezwa. Sasa anatuletea masuala mengine kuhusu ‘wilbaro’ kwa watu wa tabaka la chini.”

Bw Odinga aliwaomba Wakenya kuwa waangalifu, kwani lengo kuu la kampeni za kuwaninua ‘mahasla’ (watu maskini) inayoendeshwa na Dkt Ruto ni njama ya kuirejesha nchi katika enzi ya giza ya Vijana wa Kanu (YK-92).

Alisema vijana wengi hawana ufahamu wa kina kuhusu hali ilivyokuwa awali nchini, ambapo serikali ilikuwa ikiwahangaisha na kuwafunga jela wale waliozungumza ukweli.

“Ni wakati wa YK-92 walipotengeneza noti ya Sh500. Wangeenda kwenye mahoteli na kulewa. Wakati huo, nchi yetu ilikuwa katika hali ngumu,” akasema.

Alisema vijana wanahitaji nafasi nzuri za ajira na hayo yanaweza tu kufikiwa kupitia sera nzuri zilizo kwenye ripoti ya BBI.

You can share this post!

Adhabu ya kiboko shuleni yapingwa

Maaskofu wafunguka kuhusu corona Tanzania, wataka wananchi...