Raila atofautiana na wanaoepuka siasa kupata ‘maendeleo’

Raila atofautiana na wanaoepuka siasa kupata ‘maendeleo’

KINARA wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amewakosoa wanasiasa wa Pwani ambao wamekuwa wakisisitiza kuweka kando siasa kwa wakati huu ili kuwahudumia wananchi.

Tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti, wanasiasa wa Pwani kutoka pande tofauti za kisiasa wamekuwa wakiandaa mikutano ambapo hujadiliana kuhusu jinsi ya kushirikiana.

Baadhi ya wanasiasa waliochaguliwa kupitia vyama tanzu vya Muungano wa Azimio, hueleza kujitolea kwao kuepuka siasa ili washirikiane na serikali ya Rais William Ruto, kwa lengo la kunufaisha wakazi wa maeneo yao kimaendeleo.

Hata hivyo, akizungumza Jumamosi katika Kaunti ya Kilifi, Bw Odinga alisema misimamo ya aina hiyo haina msingi kwa vile siasa haiwezi kutenganishwa na mipango ya kimaendeleo katika jamii.

“Uongozi ni siasa. Na siasa na maendeleo ni mambo ambayo hayatenganishwi. Huwezi kusema unaacha siasa ili kufanya kazi. Siasa haiwezi kuisha,” akasema.

Bw Raila alisema serikali ya kitaifa ina jukumu la kuwahudumia Wakenya wote bila kuwabagua, na kuitaka kuzipa serikali za kaunti mgao wao bila kuvutana na kutekeleza miradi yote ya maendeleo iliyopendekezwa katika serikali za kaunti.

“Serikali ya kitaifa ina jukumu la kukusanya ushuru na kugawanya kwa serikali za kaunti. Kaunti hazifai kuanza kuombaomba fedha kutoka kwa serkali ya kitaifa,’ akasema, katika hafla ya kutoa shukrani kwa uchaguzi wa Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro.

Wanasiasa waliokuwepo katika hafla hiyo walikuwa wameendelea kuvumisha msimamo wao wa kutaka kuweka kando siasa, wakidai ni kupitia njia hiyo ambapo watafanikiwa kuleta maendeleo kwa Wapwani.

Mbunge wa Rabai, Bw Kenga Mupe, na mwenzake wa Ganze, Bw Kenneth Kazungu ambao ni wanachama wa PAA kilicho katika muungano wa Kenya Kwanza, walisema wananchi wa Kilifi wanatarajia kutatuliwa changamoto sugu kama vile njaa na uhaba wa maji.

“Hatuwezi kuendelea kuchapa siasa. Watu wa Kilifi hawatakula siasa. Ni wakati wetu viongozi kuungana na kumpa Rais William Ruto na Gavana Gideon Mung’aro wakati kuhudumia wananchi,” akasema Bw Kazungu.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia, Bi Aisha Jumwa, aliyesisitiza kuwa wakati wa siasa uliisha.

Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo (ODM), alisema ingawa wamejitolea kuungana ili kuleta maendeleo, hilo halimaanishi wataacha kutekeleza majukumu yao kama viongozi wa upinzani hasa katika Seneti na Bunge la Taifa.

Alitoa changamoto kwa wananchi wasiogope kuwakosoa viongozi wao ili watumikiwe inavyostahili.

Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, alionya viongozi wa Pwani dhidi ya kutengana akisema athari itakuwa mbaya kwa wakazi wa ukanda huo.

Bw Mung’aro alisema ataitisha mkutano wa viongozi wa Pwani hivi karibuni ili washauriane kuhusu mwelekeo wanaofaa kuchukua kwa pamoja.

Mwenzake wa Taita Taveta, Bw Andrew Mwadime, alisema walimchagua Bw Mung’aro kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani kwa sababu wana imani kwamba anaweza kuleta umoja wa Wapwani ambao umekuwa ukiwaponyoka kila mara.

  • Tags

You can share this post!

Mary Wambui Mungai kujua hatma yake Januari 10, 2023

Jumwa asisitiza azma yake ya ugavana Kilifi bado haijafa

T L