NA CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya sasa anaonekana kutorokwa na washirika wake wa karibu. Wengi wamekuwa wakikwepa mikutano yake ya kupinga serikali ya Kenya Kwanza.
Kando na magavana wote 21 waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama tanzu katika muungano huo, maafisa wakuu, wabunge na maseneta kadha wa ODM, hususan, kutoka ng’ome yake ya kisiasa ya Nyanza wamechelea kuhudhuria mikutano miwili iliyoongozwa na Bw Odinga jijini Nairobi juzi.
Miongoni mwa waliokwepa mikutano hiyo iliyoandaliwa katika viwanja vya Kamukunji na Jacaranda ni Naibu Kiongozi wa ODM Hassan Joho, Mwenyekiti John Mbadi na Mkurugenzi wa Uchaguzi Junet Mohamed, miongoni mwa wengine.
Wengine ni; kiongozi wa Narc Charity Ngilu, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.
Wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, wanasiasa hawa, haswa Joho na Mohamed, walikuwa wakiandamana na Bw Odinga kote kote kwenye mikutano yake ya kusaka kura nchini.
Bw Mohamed, ambaye ni Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, pia ni Katibu Mkuu wa muungano wa Azimio.
Tulipowasiliana naye ana kujua sababu zake kukwepa mikutano miwili iliyoongozwa na Bw Odinga, Mbunge huyo wa Suna Mashariki alitoa jibu fupi la, “Hali ni sawa”.
Lakini mara ya mwisho Bw Mohamed kuonekana hadharani na Bw Odinga ilikuwa Januari 11, 2023 alipoandamana naye kumtembelea Balozi wa Uingereza nchini, Jane Marriott.
Kwa upande wa Joho, duru zinasema Gavana huyo wa zamani wa Mombasa ameamua kujitenga na masuala ya kisiasa na kuamua kujishughulisha na biashara zake.
Kando na kumtakia Bw Odinga heri njema alipoadhimisha siku yake ya kuzaliwa, Januari 8, taarifa na picha zilizoko katika ukarasa wa Bw Joho wa Twitter zinahusu masuala ya kidini, urafiki na zile za kushabikia klabu ya soka ya Arsenal ya Uingereza.
Bw Mbadi ambaye ni Mbunge Maalum, juzi alitoa wito kwa wafuasi wa Azimio kumkumbatia Dkt Ruto kama Rais halali wa Kenya akiwataka kukoma kuamini ufichuzi kwamba Bw Odinga ndiye alishinda katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Watu wetu wa Azimio ninaomba tuachane na huu mjadala eti fulani alipata kura fulani. Tusonge mbele ili tuweze kuvuna maendeleo kwa manufaa yetu sote,” akasema katika mkutano wa hadhara katika eneo la Gwasi, eneo bunge la Suba Kusini.
Bw Mbadi, alisema hayo siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni kuweka wazi ripoti ya mfichuzi huyo iliyoonyesha Bw Odinga ndiye alishinda katika kinyang’anyiro cha urais kwa kupata kura 8,170,35 (sawa na asilimia 57.5). Mfichuzi huyo, anayedaiwa kuwa mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), anadai Rais Ruto alipata kura 5,915,973 (sawa na asilimia 46.6).
Lakini kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Rais Ruto alishinda kwa kuzoa jumla ya kura 7,176, 141 (sawa na asilimia 50.49) huku Bw Odinga akipata kura 6,942,930 (sawa na asilimia 48.85 ya kura).
Ni kutokana na madai hayo ya “ushindi” wa Bw Odinga ambapo mwanasiasa huyo mkongwe alitangaza msururu wa mikutano ya hadhara kote nchini kupinga utawala wa Dkt Ruto.
Wakati wa mkutano katika uwanja wa Kamukunji, Januari 22, Bw Odinga akasema: “Leo ninatangaza kutoka hapa Kamukunji kwamba, sisi kama Azimio hatumtambui Ruto kama Rais wa Kenya. Vile vile, hatutambui maafisa wote wanaohudumu chini yake.”
Ingawa wabunge wa ODM kutoka Nairobi, wakiongozwa na Babu Owino (Embakasi ya Kati) walihudhuria mkutano huo, wenzao kutoka Nyanza hawakuwepo.
Katika mkutano wa Jacaranda, Mbunge wa Kisumu Magharibi Rosa Buyu, ndiye wa pekee aliyehudhuria mkutano.Miongoni mwa vigogo wa Azimio waliohudhuria mkutano huo ni aliyekuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga Martha Karua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa na aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.
Hatua ya wabunge, maseneta na magavana kukwepa mikutano miwili ya Azimio, Nairobi ndio ilipelekea Bw Musyoka kutangaza kuwa wanawachunguza mienendo yao kwa makini.
“Tunawafuatilia kwa ukaribu wabunge na viongozi wengine wa Azimio waliochaguliwa ambao wanajiepusha na mikutano yetu na wanafanyakazi na Kenya Kwanza. Hii ni kwa sababu viongozi hawa wanakwenda kinyume na matakwa ya wananchi waliowachagua,” akaonya.
Lakini Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior anashikilia kuwa hatahudhuria mikutano ya Azimio huku akiapa kuendelea kuitambua serikali ya Dkt Ruto.
“Nitaendelea kushirikiana na serikali kuu inayoongozwa na Rais Ruto kwa manufaa ya watu wetu. Kamwe sitajihusisha na mikutano ya Azimio kwa sababu niko na kazi ya kuwafanyika wakazi wa Makueni,” akasema.
Magavana wengine wa Azimio ambao wameamua kufanya kazi na Serikali “katika nyanja ya maendeleo” ni Abdulswamad Nassir (Mombasa), Dkt Paul Otuoma (Busia), Wavinya Ndeti (Machakos), Julius Malombe (Kitui), Simba Arati (Kisii), James Orengo (Siaya) miongoni mwa wengine.
Subscribe our newsletter to stay updated