Habari

Raila atuliza maswali kuhusu alikokwenda baada ya kufichua yuko DRC

November 21st, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

IMEFICHUKA kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga yuko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa shughuli za kikazi kama Mjumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundomsingi.

Hayo yalifichuka Ijumaa jioni kupitia ujumbe na picha kwenye akaunti yake ya Twitter, siku moja baada ya shughuli ya ukusanyaji sahihi, za kufanikisha kura ya maamuzi kutekeleza mapendekezo kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI), kuahirishwa ghafla.

Katika picha hizo Bw Odinga anaonekana akikagua ujenzi wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme kwa njia ya maji kwa jina, Grand Inga Hydropower Project mjini Lubumbashi, DRC.

“Mradi wa umeme wa Inga Hydropower ni mojawapo ya miradi mikubwa ya miundo msingi katika mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika (AU). Nimejadiliana na Gavana wa jimbo la Katanga, Jacques Kyabula kuhusu umuhimu wa mradi huu afisini mwake jijini Lubumbashi,” akasema.

Oktoba, Bw Odinga alizuru DRC ambapo alifanya mazungumzo na Rais Felix Tshisekedi.

Lakini kabla ya kiongozi huyo wa ODM kusafiri kuenda taifa hilo, Bw Odinga alikuwa ametarajiwa kutoa sababu za kuahirishwa kwa mpango wa ukusanyaji wa angalau sahihi 1 milioni za kuunga mkono mswada wa BBI.

Hata hivyo, hakutoa taarifa zozote ila wakuu wa kamati simamizi inayoandaa shughuli hiyo walisema iliahirishwa kwa sababu mswada wa BBI haukuwa tayari.

Hata hivyo, kwa kuwa kuahirishwa kwa shughuli hiyo kulijiri saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na Naibu wake William Ruto, uvumi ulienea kwamba huenda Rais alikubali wito wa kuifanyia marekebisho ripoti hiyo.

Dkt Ruto, viongozi wa kidini na wadau wengine wamekuwa wakishinikiza kuwa ripoti hiyo ifanyiwe marekebisho ili kujumuisha mapendekezo na maoni ambayo yaliachwa nje.

Kulingana na Naibu Rais hii ndiyo njia ya kipekee ya kuhakikisha kuwa kura ya maamuzi kuhusu marekebisho ya Katiba haisababishi migawanyiko nchini.