HabariSiasa

Raila atuzwa kwa kupigania utawala bora

May 24th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga amepokea tuzo ya kimataifa kutokana na juhudi zake za kupigania utawala bora.

Tuzo hiyo kwa jina Black Entertainment Film Fashion, Television and Arts (BEFFTA) hupewa watu waliobobea katika fani mbalimbali za sanaa, michezo na masuala ya utawala katika jamii za watu w ngozi nyeusi duniani, hususan katika mataifa ya Uingereza, Amerika na Canada.

Tuzo hiyo iliasisiwa na Dkt Pauline Long, mcheza filamu mtajika, aliyesema tuzo hiyo hulenga kuwatia moyo watu weusi kote duniani ambao wamepigania haki na utawala bora.

Akiongea katika hafla ya tuzo hiyo jijini London Jumanne usiku, Bw Odinga alisema ulimwengu bado unaendelea kupongeza mwafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta ambao umetuliza joto la kisiasa nchini.

“Walimwengu wamepongeza hatua yangu ya kusalimiana na Rais Kenyatta kutokana na hali kwamba umeleta amani na maridhiano nchini kufuatia tofauti zilizoibuka kufuatia uchaguzi mkuu uliopita,” alisema.

Bw Odinga amepokea tuzo hiyo wakati ambapo mwafaka kati yake na Rais Kenyatta unakabiliwa na mawimbi ya upinzani kutoka Naibu Rais William Ruto, wakili Miguna Miguna na wakuu wa muungano wa NASA.

Ruto anapinga pendekezo la Bw Odinga la kutaka Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuubadilisha mfumo wa uongozi kupitia kubuniwa kwa nyadhifa za waziri mkuu na manaibu wake wawili.