Habari

Raila aunga mkono mfumo wa ugavi wa fedha kuzingatia idadi ya watu katika kaunti

July 27th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amesalimu amri na kuamua kuunga mkono mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA).

Kwenye taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari Jumatatu Bw Odinga amewata maseneta kusitisha mvutano kuhusu suala hilo na ambao umeendelea kwa majuma kadha.

Amewataka waruhusu matumizi ya mfumo huo mpya utakaofanya kaunti zenye idadi kubwa ya watu kutengewa fedha nyingi kuliko kaunti kubwa na zenye idadi ndogo ya watu.

Bw Odinga alikosoa maseneta kwa kufeli kukubaliana kuhusu marekebisho ambayo wangetaka yafanywe kwa mfumo uliopendekezwa na CRA.

Mvutano kuhusu huo ulikuwa umetisha kusambaratisha ukuruba kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu handisheki na mpango wa maridhiano (BBI).

Hii ni baada ya kiranja wa wengi Irungu Kang’ata kutisha kwamba Jubilee itajiondoa kutoka handisheki na BBI ikiwa ODM maseneta wa ODM wataendelea kupinga mfumo huo mpya.

Bw Odinga amewataka maseneta, wanaopinga mfumo huo, kuupitisha kisha wawasilishe mapendekezo yao kwa CRA ili yajumuishwe kwa mfumo utakaotolewa baada ya miaka mitano.

“Suala kuu katika mfumo huo wa CRA utakaotumika kwa miaka mitano ijayo ni kwamba unazingatia idadi ya watu. Umejengwa katika mantiki kuwa wajibu mkuu wa serikali za kaunti ni utoaji huduma kwa wananchini katika sekta za afya, kilimo, miundo msingi, elimu miongoni mwa mingine,”

“Seneti ilifanya mabadiliko kadha kwa mapendekezo ya CRA lakini ikadumisha kigezo kikuu kwamba ugavi wa fedha utategemea idadi ya watu. Kwa bahati mbaya bunge hilo limekosa kuafikia kuhusu marekebisho yake,” akasema Bw Odinga

Kiongozi huyo wa ODM alisema katika hali ya sasa taifa la Kenya litahudumiwa kwa njia sawa ikiwa mapendekezo ya CRA yatatumika kwa miaka mitano ijayo.

“Hii itawezesha taifa kupata nafasi ya kuelekeza jitihada zake katika vita dhidi ya corona,” Bw Odinga akasema.

Alisema mvutano kuhusu suala hilo umejivuta kwa kwa muda mrefu na hivyo kuzinyima serikali za kaunti mgao wa fedha zinazohitaji kufadhili vita dhidi ya corona na kutoa huduma kwa wananchi.

“Inasikitisha kuwa mvutano huo pia umechukua mwelekeo wa kikabila na kisiasa badala ya kuhusu masuala muhimu ya maendeleo ya taifa,” akasema Bw Odinga.

Maseneta kutoka maeneo la Kaskazini Mashariki, Kaskazini, Pwani maeneo fulani ya Nyanza wamekuwa wakipinga mfumo huo mpya ambao utapelekea takriba kaunti 18 kupoteza fedha, ikilinganishwa na mgao wao wa mwaka jana.

Na jumla ya kaunti 29 zenye idadi kubwa ya watu zitapokea nyongeza za fedha ikilinganisha na mgao wao wa mwaka jana.