Habari za Kitaifa

Raila ayataka makanisa kukemea Ruto kuhusu ‘uongozi mbaya’

January 14th, 2024 2 min read

NA JUSTUS OCHIENG

KINARA wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amelitaka kanisa liungane na Wakenya kukemea maovu ya Kenya Kwanza huku akilenga kupeleka ziara za kushauriana na raia Magharibi na Pwani wiki hii.

Bw Odinga akizungumza Jumapili, Januari 14, 2024 katika kanisa la Kianglikana la St Stephens Kisumu, aliwataka viongozi wa kanisa wawe watu wa kuzungumzia ukweli nchi ikikabiliwa na changamoto ya uongozi mbaya kama sasa.

Aliwataja marehemu Maaskofu Henry Okullu, Alexander Muge na David Gitari kama waliosimama na ukweli na kukemea maovu ya utawala wa Kanu.

“Viongozi wa makanisa wanastahili kuzungumzia maovu ya serikali hii. Maaskofu Muge, Gitari na Okullu walikuwa viongozi wa makanisa ambao walisimama na ukweli wakati ambapo ukosoaji kwa serikali ya Kanu ulichukuliwa kama hatia ya mapinduzi,” akasema Bw Odinga.

“Walizungumza na kueleza uongozi wa wakati huo ukweli. Viongozi wa makanisa wanastahili kuwaambia wale ambao wapo mamlakani kuwa wanawaumiza raia,” akaongeza.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, Seneta wa Kisumu na Naibu gavana Mathews Owili, Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga, wabunge Aduma Owuor (Nyakach), Joshua Oron (Kisumu ya Kati) miongoni mwa wanasiasa wengine.

“Kanisa linastahili kulaani ushuru wa juu ambao utawala huu umewabebesha raia. Serikali inahadaa watu kwa kusema inataka kuondoa nchi kwenye madeni ilhali bado inakopa,” akasema Kiongozi huyo wa upinzani.

Kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa kanisa na siasa hazina tofauti kwa hivyo viongozi wa dini hawafai kuogopa kujitokeza na kukosoa serikali.

“Si Zakayo pekee yake alikuwa akitoza ushuru bali kuna hata Mathayo na hakuna tatizo katika kukusanya ushuru. Kosa ni kuwa wanaongeza ushuru kisha pesa hizo zinaporwa.

“Wakati mwingine naaibika kuona viongozi wa ACK, ambalo ni kanisa langu wamenyamazia maovu yanayoendelea. Ninafurahia jukumu ambalo wenzetu Wakatoliki wanatekeleza kupinga maovu ya serikali. Inasikitisha kuwa watu ambao wamekuwa wakijifanya Wakristo ndio baada ya kutwaa mamlaka, wamekuwa wakinyanyasa raia kwa kuongeza ushuru,” akasema.

Bw Odinga atakuwa ziarani kwenye kaunti tisa kuandaa mikutano na raia na kushauriana nao huku duru zikiarifu kuwa upinzani huenda ukarejelea maandamano kupinga kuongezwa kwa ushuru.

Bw Odinga anasema kuwa atatoa mwelekeo mpya kuhusu jinsi upinzani utashinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha.

Mikutano hiyo pia itatumiwa kuendeleza usajili wa wanachama wa ODM katika maeneo ya Magharibi na Pwani.

Jumapili, alikuwa katika Kaunti ya Busia ambako alianza ziara yake ukanda wa Magharibi.

Jumatatu, Bw Odinga atakuwa kwenye mikutano ya kuwasajili wanachama wa ODM kaunti ya Vihiga kabla ya kuelekea Bungoma mnamo Jumatano.

Mnamo Januari 22, ataandaa mkutano wake wa kwanza kisiwani Lamu kabla ya kuekekea Tana River na Kilifi.

Baada ya hapo ataelekea Taita-Taveta, Kwale kisha kuhitimishia ziara hiyo Mombasa.

Katibu wa ODM Edwin Sifuna alisema mikutano hiyo itakuwa inaongozwa na Bw Odinga mwenyewe, maafisa wakuu wa ODM na pia viongozi waliochaguliwa.

Disemba 30, 2023 Bw Odinga alitoa wito kwa serikali iondoe Sheria ya Fedha 2023 la sivyo awaongoze wafuasi wake kurejea barabarani kwa maandamano.