Habari Mseto

Raila azidisha kampeni za kuwania wadhifa wa AUC

May 1st, 2024 2 min read

NA JUSTUS OCHIENG

MWONGOZO wa kampeni za Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, kuhusu azma yake ya kuwania wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) umetolewa.

Taifa Leo imebaini kuwa kinara huyo wa Azimio la Umoja One Kenya ameorodhesha misururu ya mahojiano yanayojumuisha kushirikisha wajumbe na wakazi katika jiji kuu la Nairobi.

Mikakati hiyo inajumuisha kukutana na wadau kutoka nje huku timu yake ikipanga kushiriki kikao na mabalozi 28 na Makamishna Wakuu jijini Nairobi.

Timu ya kampeni ya Bw Odinga inayoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mamlaka kuhusu Maendeleo Baina ya Serikali (IGAD), Mahboub Maalim, na aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Amerika, Elkanah Odembo, imepanga mikutano ya kampeni na wajumbe wote wa kigeni Mei na Juni ili kuomba uungwaji mkono kutoka kwa mataifa yao.

“Balozi Mahboub Maalim nami binafsi tutawatembelea tukianza na Balozi wa taifa la Eritrea ambaye ni Msimamizi wa Mabalozi Waafrika,” Bw Odembo alieleza Taifa Leo.

“Ziara hizi zinadhamiriwa kuendelea kumpigia debe mgombea wa Kenya.”

Alisema ziara hizo vilevie zinakusudiwa kujua ikiwa nchi fulani inamezea mate wadhifa wowote wa kimataifa.

“Hii ni muhimu ili tuhakikishe Kenya inaonyesha shukran kwa kuunga mkono azma yao,” alisema.

Bw Odembo alisema ni muhimu kutilia maanani mahitaji na maslahi ya mataifa mengine ya Afrika.

“Hatujatilia maanani suala hili katika juhudi zetu za awali. Hatua ya kurejesha mkono ni muhimu katika masuala ya kimataifa na ya kidiplomasia.”

Rais William Ruto tayari ameimarisha nafasi ya Bw Odinga kugombea nchini Ghana miongoni mwa mataifa mengine ya Afrika. Alipozuru Ghana mwezi uliopita, Dkt Ruto alimpongeza Rais Nana Akufo-Addo kwa kukubali kuunga mkono azma ya Kenya kuhusu AUC.

Kama ishara ya kushukuru, Rais Ruto alikubali kumuunga mkono Waziri wa Masuala ya Kigeni nchini Ghana, Shirley Ayorkor Botchwey, kuwania wadhifa wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola katika chaguzi zitakazofanyika nchini Samoa katika mkutano wa Viongozi wa Serikali za Jumuiya ya Madola 2024.

Bw Odinga alisafiri nje ya nchi Jumatatu usiku, baada ya kushiriki mazungumzo na Rais wa Benki ya Ulimwengu, Ajay Banga, kuhusu mustakabali na uwezo wa Afrika kiuchumi.

Huku akiandamana na Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed, kiongozi huyo wa ODM aliondoka nchini kwa shughuli fupi ya kidiplomasia huku akipangiwa kurejea baadaye wiki hii.

Bw Odinga alikuwa amehudhuria Kongamano la Kimataifa la Benki ya Dunia (IDAs) kuhusu Viongozi wa Mataifa na Serikali za Afrika lililofanyika jijini Nairobi na kuhudhuriwa pia na viongozi 19 wa bara hili.

Wajumbe waliohudhuria hafla hiyo walijumuisha vilevile muungano wa vijana, sekta ya kibinafsi, na wanaharakati walioahidi kujitolea upya kufanikisha ustawishaji wa maendeleo Afrika.

Bw Odinga alichukua fursa hiyo kujipigia debe kuhusu wadhifa huo wa uongozi barani.