Habari

Raila azungumzia haja ya Katiba kufanyiwa marekebisho

August 10th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amesema Katiba nzuri ni ile inayoweza kurekebishwa ili ikidhi mahitaji ya raia na wakazi wa nchi.

Pia ameelezea kushangazwa kwake na baadhi ya viongozi na wanasiasa ambao kwa mtazamo wake wanapinga mabadiliko ya Katiba ya sasa na iliyoidhinishwa 2010.

Waziri huyo mkuu wa zamani kwenye mahojiano na runinga ya NTV inayomilikiwa na Shirika la Nation Media Group (NMG), alisema wanaopinga mabadiliko ya Katiba kutekelezwa ni “walewale waliodai si bora”.

Bw Odinga alisema “huo ni unafiki wa hali ya juu kupinga mageuzi, ilhali ilipoidhinishwa haikuwaridhisha”.

Kiongozi huyo wa upinzani na ambaye kwa sasa anashirikiana kwa karibu na serikali ya Jubilee, baada ya salamu za maridhiano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta maarufu kama Handisheki, mnamo Machi 2018, alisema wanaokataa mabadiliko wanaongozwa na tamaa za ubinafsi.

“Wanaokataa mabadiliko ya Katiba, ni walewale waliopinga ipitishwe 2010. Huo ni unafiki wa hali ya juu na nasema kwamba wanaongozwa na tama na ubinafsi,” Bw Odinga akaambia Mkurugenzi wa Uhariri wa NMG Bw Mutuma Mathiu.

Raila Odinga alitoa kauli hilo kufuatia swali la Bw Mutuma kuhusu pendekezo la mabadiliko ya Katiba, katika mapendekezo ya ripoti ya tume ya maridhiano, BBI.

Licha ya janga la Covid-19 kutatiza na kusimamisha shughuli nyingi, ikiwamo hamasisho la BBI, kiongozi huyo wa ODM alisema haoni kizingiti chochote katika maandalizi ya kura ya maoni kufanyia marekebisho katiba ya sasa, kabla mwishoni mwa mwaka huu wa 2020.

Kuhusu pendekezo la kura ya maoni kuandaliwa pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Odinga alisema hilo litaleta mkanganyiko mkuu kwa wapiga kura. “Uchaguzi unashirikisha nyadhifa sita, kuongeza kura ya maoni italeta mkanganyiko mkuu,” akaelezea.

Alisema mabadiliko ya Katiba ya Kenya yamechukua muda mrefu kutekelezwa ilhali mataifa mengine yalifanya miezi michache baada ya kuidhinishwa.

“Katiba ya Amerika ilikarabatiwa miezi michache baada ya kuidhinishwa kutumika, pia ya Ufaransa. Yetu (Kenya) inarekebishwa miaka 10 baadaye,” Raila akasema, akieleza kwamba mabadiliko yanayolengwa yananuwia kuimarisha maisha ya wananchi.

Tangu kufanyika kwa Handisheki Machi 2018, uhusiano kati ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto umeonekana kuzorota.

Salamu za maridhiano zilipelekea kuibuka kwa kundi la ‘Kieleweke’ linaloegemea upande wa Rais Kenyatta na Bw Raila, na ‘Tangatanga’ linaloegemea upande wa Naibu Rais.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakilalamikia kutengwa kwa Naibu Rais kwenye shughuli za serikali, wakidai Raila ndiye kiini cha nyufa katika mrengo tawala wa Jubilee.

Aidha, ‘Tangatanga’ wamekuwa wakitilia shaka uhalali wa BBI, viongozi hao wakisema tume hiyo iliundwa kuzima ndoto za Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022. Kundi hilo pia limekuwa likipinga pendekezo la kuandaa kura ya maoni, likisema mabadiliko yanaweza kufanywa bungeni.

Mabadiliko ya Katiba yanaweza kufanywa kwa njia tatu; Kupitia bunge, Afisi ya Rais na kupitia kura ya maoni inayohusisha kila mwananchi.