Habari

RAILA: BBI hailengi kubadilisha Katiba

September 7th, 2020 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

KINARA wa ODM, Raila Odinga, amesema kuwa Mpango wa Maridhiano (BBI) haulengi kuifanyia mageuzi Katiba, lakini lengo lake kuu ni kutatua changamoto ambazo zinawaathiri Wakenya.

Akihutubu nyumbani kwa Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya, alipokutana na viongozi wa ODM kutoka eneo la Magharibi jana Jumapili, Bw Odinga alisema kuwa baadhi ya vipengele vya Katiba vitahitaji kuwasilishwa kwenye Bunge la Kitaifa ili kujadiliwa kabla ya kupitishwa.

Hata hivyo, vipengele vingine vitahitaji kuwasilishwa kwa wananchi kupitia kura ya maamuzi.

“Ripoti ya BBI hailengi kuifanyia mageuzi Katiba lakini kutoa suluhisho kwa matatizo yanayowaathiri Wakenya kijumla. Tunataka kujua jinsi jamii zinavyoweza kuishi na kukubaliana bila tofauti zozote miongoni mwao,” akasema.

Alisema ripoti hiyo itatoa mwongozo kuhusu vipengele vitakavyohitajika kuwasilishwa Bungeni ili kutathminiwa upya.

Bw Odinga alieleza kuwa baadhi ya vipengele vinaweza kutekelezwa vile tu vilivyo kwenye Katiba, lakini Serikali ya Kitaifa na zile za kaunti hazijakuwa zikivitekeleza.

Kwenye hotuba yake, alisema Katiba ya sasa siyo Wakenya waliotaka mnamo 2010, lakini hawakuwa na chaguo lingine ila kuikubali ilivyo.

“Ni kwa sababu hiyo nilifanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta ambapo tulikubaliana kiunganisha nchi. Tuliamua kupokea maoni ya Wakenya wote ili kuiboresha Kenya na kuifanya mahali bora kila mmoja anaweza kukaa bila tatizo lolote,” akasema.

Hata hivyo, alisisitiza kuhusu haja kuhusu utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi, akisema Katiba ya sasa iliingiliwa hivyo kukosa kuifanya kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Ziara yake ilionekana kama juhudi za kurejesha umaarufu wa kisiasa wa ODM katika eneo hilo, hasa mvutano baina yake na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi unapoendelea kutokota.

Wawili hao wameanza juhudi kali kupigania udhibiti wa kisiasa wa eneo hilo, baada ya muungano wa Nasa kusambaratika.

Hili linafuatia hatua ya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Chama cha Mashinani (CCM), Isaac Rutto kutia saini mkataba wa kisiasa na Chama cha Jubilee (JP).

Jumamosi usiku, Bw Odinga alifanya mazungumzo na viongozi kutoka eneo hilo ambapo baadaye alikutana na madiwani wa ODM kutoka kaunti hiyo nyumbani kwa Bw Oparanya, katika kijiji cha Emabole, eneo la Butere.

Gavana Wycliffe Wangamati (Bungoma), wabunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), Godfrey Osotsi (mbunge maalum) walihudhuria kikao cha Jumamosi huku mwenzao Justus Kizito (Shinyalu) akihudhuria mkutano wa Jumapili.

Bw Odinga alisema watafanya uchaguzi wa mashinani katika kaunti hiyo ili kuhakikisha imeendelea kuwa ngome kuu ya ODM.

“Tulikuwa tumepanga kufanya chaguzi hizo kuanzia Machi hadi Juni lakini mipango hiyo iliathiriwa na janga la virusi vya corona. Hata hivyo, tumeanza kuweka mikakati kukipa umaarufu chama tena mashinani,” akasema.

Bw Oparanya alimhakikishia Bw Odinga kuwa eneo hilo bado linaendelea kumuunga mkono kama ambavyo limekuwa likifanya kwenye chaguzi za hapo awali.