Raila: DCI haiwezi kufanya uchunguzi huru kwa sababu Amin ni ‘mfanyakazi wa Ruto’

Raila: DCI haiwezi kufanya uchunguzi huru kwa sababu Amin ni ‘mfanyakazi wa Ruto’

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga sasa anasema kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) haiwezi kuchunguza udanganyifu katika uchaguzi anaodai ulichangia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Akiongea baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Jesus Teaching Ministry mtaani Donholm, Nairobi, Januari 29, kiongozi huyo wa Azimio la Umoja-One Kenya alisema uchunguzi huo hautakuwa huru na utaekelezwa na Serikali Kuu.

Bw Odinga alisema kuwa hana imani kwamba Mkurugenzi Mkuu wa DCI Mohamed Amin ataendesha uchunguzi huo kwa njia ya ‘haki’ kwa sababu afisa huyo aliteuliwa na Rais William Ruto.

“Nasikia eti yule DCI anataka kufanya uchunguzi kuhusu wizi wa kura. Bw DCI wewe ni mwajiri wa Bw Ruto na hauwezi kufanya uchunguzi huru na wa haki,” Bw Odinga akasema.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema hayo kabla ya kuelekea katika uwanja wa Jacaranda ambako aliongozwa mkutano mkubwa wa kisiasa kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza.

Afisi ya DCI Amini imeanzisha uchunguzi kuhusu madai kuwa Rais Ruto hakushinda kwa njia halali katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Afisa huyo ameripotiwa akisema kuwa afisi yake imepokea malalamishi kwamba hesabu za kura katika baadhi ya fomu 34B kutoka maeneobunge 290 zilivurugwa.

“Katika siku chache zilizopita DCI imepokea barua nyingi na malalamishi kutoka kuhusiana na habari zinazosambazwa mitandaoni zinazohusishwa na IEBC,” Bw Amin akasema kwenye barua kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan.

“Aidha, tumepata stakabadhi zenye hesabu zinazodaiwa kuwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais,” DCI ataongeza.

Alisema kuwa Idara hiyo inachunguza uhalali wa stakabadhi hizo pamoja na ikiwa stakabadhi rasmi za IEBC zilighushiwa na kuvurugwa kinyume cha sheria au tararibu zilizowekwa.

Bw Amin aliomba IEBC kuwapa maafisa wake nakala rasmi za Fomu 34B zilizotumiwa kutangaza matokeo ya urais.

Aliongeza kuwa mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kughushi Fomu 34B na kuzichapisha maelezo kuzihusu kuendeleza madai ya uwongo atakabiliwa na mkono wa sheria.

“Ikiongozwa na sheria, DCI ina wajibu wa kushughulikia masuala yaliyoibuka na kuendesha uchunguzi wa kina na kitaalamu,” Amin akasema.

Kwa mujibu wa sheria mtu atakayepatikana na hatia ya kuchapisha habari za uwongo anaweza kuadhibiwa kwa kutozwa faini isiyozidi Sh5 milioni.

Kulingana na Sehemu za 22 na 23 za Sheria hiyo ya kudhibiti matumizi mabaya na uhalifu wa kimtandao, 2018, mtu kama huyo akifeli kulipa faini hiyo atafungwa jela kwa kipindi kisichozidi miaka 10.

Mnamo Januari 18, 2023, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alidai kuwa Bw Odinga ndiye alishinda katika uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema madai yake yanatokana na ufichuzi ulitolewa na mtu fulani aliyedai kuwa mfanyakazi wa IEBC na “aliyeamua kuweka maisha yake na ya familia yake hatarini kwa ajili ya kusimamia ukweli.”

  • Tags

You can share this post!

Raila amtemea Ruto moto kuhusu kura

PAUKWA: Ujanja wanusuru Msanii asifutwe kazi na Kaburu

T L