Habari MsetoSiasa

Raila hajaenda ng'ambo kwa matibabu – ODM

June 24th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM kimekanusha uvumi kuwa kinara wake Raila Odinga amepelekwa ng’ambo kwa matibabu.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, aliwataka Wakenya kupuuza uvumi huo akiutaja kama usio na msingi. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu aliko Bw Odinga.

Lakini meneja wa mawasiliano wa ODM, Philip Etale, alisema kuwa Bw Odinga alikuwa jijini Kinshasa, DRC kuhudhuria kongamano kuhusu bwawa kubwa la Inga.

Hata hivyo hakuweka picha kutangaza uwepo wake katika mkutano huo ilivyo kawaida yake anapofahamisha Wakenya matukio muhimu.

Uvumi kuwa Bw Odinga ni mgonjwa na alisafirishwa Abu Dhabi kwa ndege ya kukodisha, yalienea mitandaoni kuanzia Jumatatu.

Ilidaiwa alikuwa apitie Abu Dhabi ili kupata ndege ya kwenda India au China.