Habari

Raila hatoshi mboga – wabunge

August 17th, 2019 2 min read

Na GEORGE MUNENE na SHABAN MAKOKHA

WABUNGE 32 wanaounga Naibu Rais William Ruto kuwania urais mwaka 2022, sasa wanamtaka kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga astaafu, wakisema muda wake siasani umekwisha.

Wabunge hao wanawake wanaojulikana kama ‘Inua Mama’ walisema Ijumaa kwamba, mchango wa Bw Odinga katika siasa za Kenya umemalizika.

Wakizungumza katika Shule ya Upili ya Kagio, Kaunti ya Kirinyaga, viongozi hao walisema kwamba Dkt Ruto ndiye kiongozi anayefaa zaidi kuwania urais mwaka 2022.

Wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo katika Bunge la Kitaifa, Bi Purity Wangui Ngirichi, walimwambia Bw Odinga anapaswa kustaafu kutoka siasani, na kumwacha Dkt Ruto.

Walimlaumu Waziri Mkuu huyo wa zamani kwa kutumia baadhi ya wabunge wa Chama cha Jubilee (JP) kumshambulia Dkt Ruto ili kuzua taswira kwamba hana umaarufu wowote katika eneo la Kati.

Walisisitiza kwamba Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto wana mkataba wa kisiasa ambao haupaswi kuvunjwa na yeyote.

Wakati wa kampeni, Rais Kenyatta aliwahakikishia Wakenya kwamba naibu wake atachukua usukani baada ya kipindi chake cha miaka kumi kuisha.

Hivyo, tunamuunga mkono Dkt Ruto na hatutamuunga mtu mwingine kuwania urais,” akasema Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti Kaunti ya Uasin Gishu Bi Gladys Shollei.

Wabunge hao walipuuzilia mbali Jopo la Maridhiano (BBI) ambapo waliwarai Wakenya wakatae mapendekezo ya mageuzi ya Katiba litakayotoa.

Waliilaumu Serikali kwa kutumia mamilioni ya pesa kufadhili shughuli za jopo hilo, walilodai liliandaa vikao vyake katika mikahawa ya bei ghali badala ya kusikiliza maoni ya Wakenya.

BBI

Badala ya BBI, waliwarai Wakenya kuunga mkono Mswada wa Punguza Mizigo wa Dkt Ekuru Aukot wa chama cha Thirdway Alliance.

Lakini wenzao wa kundi la ‘Embrace’ waliwarai Wakenya kuunga mkono mapendekezo yatakayojitokeza kwenye ripoti ya BBI.

Wakihutubu katika Kaunti ya Kakamega, viongozi hao walisema kwamba hiyo ndiyo njia ya pekee itayoihakikishia Kenya ufanisi wa kisiasa.

“Kama kundi la Embrace; tunaunga mkono mapendekezo ya kuifanyia mageuzi Katiba kwa lengo kuwa hayataondoa haki za wanawake zilizopo, akasema Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kakamega katika Bunge la Kitaifa, Bi Elsie Muhanda.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko alisema kwamba lengo la kundi hilo ni kuhubiri amani katika sehemu mbalimbali nchini.

Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi Bi Esther Passaris na mwenzake wa Homa Bay Gladys Wanga, waliokosoa vikali Mswada wa Punguza Mizigo.

Walisema kuwa mswada huo haujaelezea njia ambazo zitaweza kutumiwa kukabili ufisadi na ukabila ambazo ni changamoto kuu nchini.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Seneta Maalum Gertrude Musuruve, Naomi Shiyonga, Mbunge wa Wajir Fatuma Gedi, Florence Mutua (Busia) na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi anayekabiliwa na changamoto City Hall, Beatrice Elachi.