Habari MsetoSiasa

Raila hawezi kuchangia maendeleo – Tangatanga

April 14th, 2019 1 min read

PETER MBURU na DPPS

WABUNGE wa vuguvugu la Tanga Tanga linalounga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022, Jumamosi waliendelea kumshambulia kinara wa ODM Raila Odinga, wakisema hana manufaa yoyote kwa maendeleo ya nchi.

Wabunge hao walionya kuwa juhudi za Bw Odinga kutaka ‘kuvunja’ chama cha Jubilee zitaambulia patupu, wakiungwa mkono na Dkt Ruto ambaye alisisitiza kuwa hakuna atakayeharibu mpango wa Jubilee wa kuunganisha Wakenya.

“Jubilee haitavunjwa na propaganda. Tutatetea umoja wa nchi yetu na sifa ya maendeleo ya serikali,” akasema Dkt Ruto.

Jumla ya viongozi zaidi ya 15 walikuwa katika hafla hiyo eneo la Mauche, Njoro, Kaunti ya Nakuru jana, wakiwemo magavana Ferdinand Waititu (Kiambu) na Joyce Laboso (Bomet), maseneta Susan Kihika (Nakuru) na Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na wabunge Charity Kathambi (Njoro), Mishra Kiprop (Kesses), Kareke Mbiuki (Maara), Kimani Ngunjiri (Bahati), Aisha Jumwa (Malindi) na David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki).

Bw Ngunjiri alilaumu Bw Odinga kuwa alikuja kuwatenganisha Rais na naibu wake, akisema hana maana.

“Hatutaruhusu utengano wowote kuletwa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto,” akasema mbunge huyo wa Bahati.

Bw Mbiuki alidai kuna watu wanaofanya mikutano kuhakikisha Rais hamuungi mkono Dkt Ruto katika uchaguzi ujao.

“Mikutano ya usiku na kumbi za mazungumzo haitasimamisha maelewano ya Rais na naibu wake. Tutahakikisha wanasalia kuwa wameungana ili kubadili Kenya zaidi,” akasema mbunge huyo wa Maara.