Habari

'Raila, Kalonzo wafaa kustaafu'

September 29th, 2019 2 min read

Na JUSTUS WANGA

ALIYEKUWA Seneta wa Kaunti ya Machakos Johstone Muthama sasa anasema wakati umefika kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka kuamua ikiwa wakati wao wa kustaafu siasa umefika.

Bw Muthama anasema japo Raila amesaidia nchi hii kupata mageuzi makubwa kidemokrasia na kikatiba, anafaa kujiuliza iwapo huu si wakati wake wa kustaafu.

“Siwezi kumwambia aliyekuwa waziri mkuu na aliyekuwa makamu wa rais kustaafu lakini huwa unafika wakati mtu anajiuza, je, ni mimi ninayefaa kuwa kiongozi? Kunaweza kuwa na mtu mzuri kuniliko? Ninaamini kama kiongozi, unaweza kufahamu wakati watu wanataka uendelee na wakati wamechoka nawe. Hatufai kupuuza hisia za watu,” alisema Bw Muthama kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Hata hivyo, aliongeza kuwa iwapo Bw Odinga angestaafu wakati huu, anaweza kuacha pengo lisiloweza kuzibwa haraka. “Raila ndiye tegemeao letu,” alisema.

Kuhusu muafaka wa Bw Odinga na Rais Kenyatta, Bw Muthama alimlaumu kiongozi huyo wa chama cha ODM kwa kufifisha upinzani.

“Muafaka uliua upinzani. Tulipaswa kukosoa Uhuru kama Rais na kupiga darubini serikali yake. Kwa sasa, serikali inafanya inachotaka,” alisema.

Bw Muthama alikuwa mmoja wa viongozi wa Muungano wa NASA ambao waliteua Odinga kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, Musyoka akiwa mgombea mwenza wake.

Alikosoa wanaoshinikiza mageuzi ya kikatiba kubuni wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake akisema, haitakuwa suluhisho la tatizo la ukosefu wa ushirikishi serikalini.

“Kubuniwa kwa wadhifa huo kutagawanya nchi zaidi. Unapobuni nyadhifa, zitatwaliwa na watu mashuhuri kutoka makabila makubwa kama Wakikuyu, Wakalenjin, Waluhya, Waluo na Wakamba na sio makabila madogo. Ninaweza kufurahia iwapo kupitia mfumo huo mtu kutoka jamii ya Ogiek atakuwa rais wa nchi hii lakini ukweli wa mambo ni kuwa, hilo haliwezekani kwa sasa,” alisema.

Kulingana na Bw Muthama, kubadilisha katiba kubuni nyadhifa kwa sababu ya watu binafsi, kunatoa mwelekeo mbaya ambapo katiba inaweza kuwa ikibadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Kujiongeza mishahara

Mwanasiasa huyo anasema mabadiliko yanayofaa ni ya kuzuia wabunge kujiongeza mishahara wanapotaka na kuhusu umiliki wa ardhi,

Kulingana na Bw Muthama, hakuna Mkenya anayefaa kumiliki zaidi ya ekari 10 za ardhi.

Japo muafaka ulituliza nchi, Bw Muthama anasema biashara zake zimeathirika baada ya kupokonywa leseni na serikali.

“Serikali haijali kwamba nimeajiri watu wengi kupitia kampuni zangu na kwamba, ninailetea nchi hii pesa nyingi kupitia ulipaji kodi,” asema.

Analaumu serikali kwa ubaguzi ilipotenganisha kesi ya uchochezi inayomkabili na wanasiasa wengine ambao waliachiliwa wiki hii.

Alikuwa ameshtakiwa pamoja na wabunge Junet Mohammed, Aisha Jumwa, Florence Mutua na aliyekuwa mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire ambao waliachiliwa huru wiki jana.