Raila kifua mbele Pwani akiungwa mkono na magavana watano

Raila kifua mbele Pwani akiungwa mkono na magavana watano

VALENTINE OBARA na ?MAUREEN ONGALA

MAGAVANA wa kaunti tano za eneo la Pwani wanapigwa darubini kisiasa kuona ikiwa watamwezesha Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kudumisha umaarufu wake katika ukanda huo.

Eneo hilo lililo na takriban wapigakura milioni mbili waliosajiliwa kufikia sasa, ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo huvutia ushindani mkubwa wa wagombeaji wa kiti cha urais kila mwaka wa Uchaguzi Mkuu.

Tangu mwaka wa 2018 wakati Bw Odinga alipoafikiana na Rais Uhuru Kenyatta, ngome yake ya kisiasa Pwani ilitikiswa baada ya Naibu Rais William Ruto kupenya na kunasa idadi kubwa ya wanachama wa ODM.

Bw Odinga alipigwa jeki wikendi baada ya Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kikiongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kuanza rasmi kampeni za kumpigia debe katika Kaunti ya Kilifi.

Bw Kingi ni mmoja wa wanasiasa walioasi chama cha ODM.

Magavana wengine wanaoegemea upande wa kinara huyo wa Muungano wa Azimio la Umoja ni Hassan Joho (Mombasa), Dhadho Godhana (Tana River), Granton Samboja (Taita Taveta) na Fahim Twaha (Lamu).

“Safari ya PAA inalenga kupeleka Pwani hadi Ikuluni. PAA imekuja kuandaa njia ya kuelekea Ikuluni, na kwa vile tunataka urais 2027, lazima tuanze safari yetu mapema,” akasema Bw Kingi, akihutubu katika eneo la Matanomane, eneobunge la Ganze.

Licha ya kuunga mkono azimio la Bw Odinga, alisisitiza kuwa Pwani itakuwa salama tu ikiwa kutakuwa na wabunge wengi watakaochaguliwa kupitia kwa chama kilicho na mizizi yake eneo hilo.

Miongoni mwa magavana wote sita wa Pwani, Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya pekee, ambaye ni mwanachama wa Jubilee ndiye anaegemea upande wa Dkt Ruto.

Mabw Mvurya, Joho na Kingi wanatumikia vipindi vyao vya mwisho kikatiba vya ugavana.

Bw Samboja ambaye alichaguliwa kupitia kwa Chama cha Wiper amekuwa akijihusisha zaidi na ODM kuliko chama chake kwa muda mrefu tangu alipochaguliwa 2017.

Uamuzi wake wa kuegemea ODM ulisababisha manung’uniko miongoni mwa baadhi ya wanachama ambao wanaamini tikiti ya kuwania ugavana inafaa kuendea ‘mwanachama mwaminifu’.

Tikiti hiyo inawaniwa pia na mbunge wa Mwatate, Bw Andrew Mwadime, ambaye amehudumu vipindi viwili tangu 2013 kupitia chama hicho.

Alipozuru kaunti hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Bw Odinga alijaribu kutuliza uhasama ambao unahofiwa huenda ukagawanya wafuasi wake kwa sababu ya ujio wa Bw Samboja.

“Hawa wote ni watu wangu. Nitawaketisha chini tuongee, na tutaelewana,” akasema.

Bw Joho awali alitaka kuwania urais kupitia ODM lakini akaamua kumwachia Bw Odinga nafasi hiyo huku akilenga nyadhifa nyingine za kitaifa endapo chama hicho kitafanikiwa kuunda serikali.

Mwezi uliopita, Bw Odinga aliunga mkono azma ya Bw Joho kujitosa katika siasa za kitaifa.

“Hakuna siku moja ambayo Hassan Joho amenisaliti. Yeye amesimama imara wakati kuna vita kali zaidi. Wengine walikuja wakamshambulia badala ya kunishambulia mimi. Sasa anamaliza kipindi chake cha ugavana Mombasa nami nimekuja kuwaomba mkubali niende naye huko juu,” akasema katika mkutano na viongozi wa kijamii mjini humo.

  • Tags

You can share this post!

Mvutano kuhusu fidia kikwazo kwa mradi wa Sh36 bilioni Pwani

Serikali kufanya mageuzi katika kilimo cha viazi

T L