Habari MsetoSiasa

Raila kuandamana na Uhuru China kukopa mabilioni ya SGR

April 21st, 2019 1 min read

Na VICTOR RABALLA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga Jumapili alitangaza kuwa, ataandamana na Rais Uhuru Kenyatta kuelekea China, kutafuta mkopo wa mabilioni ya pesa, kuendeleza ujenzi wa reli ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Bw Odinga alisema ziara hiyo ya Beijing itatoa nafasi kwa mkopo wa Sh350 bilioni kupatikana, ili kufadhili ujenzi wa reli hiyo ambayo itafufua bandari ya Kisumu, iliyokuwa imeanguka kutokana na hali ya reli ya sasa kutofanya kazi.

Matamshi yake yamekuja baada ya kundi la maafisa wakuu katika serikali, kutoka wizara ya Fedha, shirika la reli, wizara ya Uchukuzi na idara ya sheria ya serikali wiki jana kukutana kukamilisha mazungumzo kuhusu zoezi hilo la kukopa.

“Nitakuwa pamoja na maafisa watakaosafiri na Rais katika nchi hiyo wiki ijayo. Reli mpya ya SGR itajengwa kutoka Naivasha, Narok, Bomet, Sondu hadi Kisumu,” Bw Odinga akaeleza wananchi, alipokuwa akiwahutubia jana katika kituo cha kibiashara cha Sondu kwenye mpaka wa kaunti za Kisumu na Kericho.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa njiani kuelekea mazishi katika kijiji cha Wanda, eneo la Nyakach alisema ujenzi wa reli hiyo ukikamilika, jiji la Kisumu litafaidika, na bandari hiyo kufunguliwa tena baada ya kukosa kufanya kazi kwa miaka mingi.

“Tutaimarisha Jiji la Kisumu kiuchumi na kulifanya kuwa imara katika soko la Afrika Mashariki,” akasema.

Kulingana na ripoti ya utendakazi ya Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) 2018, bandari hiyo ya Kisumu iliyoanzishwa 1901 imeshughulikia tani 12,000 za mbolea pekee ambazo zilisafirishwa hadi Uganda, tani 240 za Magadi Soda, tani 108 za mashine nzito zilizokuwa zikielekea Tanzania na tani mbili za vifaa vingine.

Bandari hiyo aidha imeingiza tani 1,100 za sukari kutoka Uganda na tani 50 za malori kutoka Dar es-Salaam, hali inayoashiria kutotumika kwake kufadhili usafiri baina ya mataifa matatu ya Afrika Mashariki.