Raila kuhudhuria uzinduzi wa chama cha PAA

Raila kuhudhuria uzinduzi wa chama cha PAA

Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA), kinachohusishwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi, kinapanga kufanya kazi na kile cha Orange Democratic Movement (ODM).

Mbunge wa Magarini, Bw Michael Kingi, alisema chama hicho kitazinduliwa mwishoni mwa mwezi huu ambapo Kinara wa ODM Raila Odinga anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Akiungumza na Taifa Leo, Bw Michel, ambaye ni kakake Gavana Kingi, alisema kwa sasa chama hicho kipya kinaendelea kusajili wanachama kote nchini.

“PAA ni chama cha kitaifa. Tuna ofisi zaidi ya 30 nchini na wananchi wengi wanazidi kujitokeza kujiandikisha kila siku,” akasema mbunge huyo wa chama cha ODM.

Aliwakosoa wanasiasa wa Pwani wanaosusia chama hicho na kung’ang’ania kile kingine kipya cha United Democratic Alliance (UDA).

Chama cha UDA kinahusishwa na Naibu Rais Dkt William Ruto, na tayari kinaungwa mkono na wanasiasa kadhaa wa Pwani.

Baadhi yao ni wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Hatibu Mwashetani (Lunga Lunga), Mohamed Ali (Nyali) na Owen Baya (Kilifi Kaskazini).

“Viongozi wote wanaodai kupigania masuala ya wapwani na wakazi wa Kilifi kupitia vyama vingine, wanafanya hivyo kwa manufaa yao wenyewe.

“Wajitokeze wazi watueleze uzuri wa vyama wanavyounga mkono. Je, ni kwa makusudi ya kibinafsi ama ya wapwani kwa jumla,” akasema.

Bw Kingi alisisitiza kuwa wengi wa viongozi hao wameweka mkataba na vyama hivyo kwa manufaa yao.

“Itakuwa tofauti kama utaweka mkataba na chama kama mtu binafsi kwa sababu utafaidika peke yako. Hata mimi nilikuwa niweke mkataba na chama cha UDA kwamba nitakuwa waziri lakini sina haja nayo,” alifichua Bw Kingi.

PAA inatarijiwa kuwakilisha Pwani katika masuala ya kisiasa na maendeleo katika serikali ya kitaifa.

“PAA inapigiania Pwani yote na sio mtu mmoja. Kila jimbo lina mwakilishi wake, hivyo itakuwa vizuri pia kwa eneo la Pwani kuwa na mwakilishi,” akaeleza.

Alikanusha madai ya Bw Baya kwamba Gavana Kingi anapanga njama ili kuendelea kubaki uongozini, na kupora mali za kaunti kupitia chama chake kipya cha PAA.

Badala yake Mbunge huyo wa Magarini alisisitiza kuwa ni UDA, inayoungwa mkono na Bw Baya, ambayo haina mazuri yoyote ya kuwapa wapwani.

“Yeye Baya anapigia debe UDA usiku na mchana kwa sababu ameahidiwa mambo mazuri.

“Haitakuwa hatia kwa Gavana Kingi kutumia chama cha PAA kutawala eneo la Pwani,” akasema.

Gavana Kingi yuko katika hatamu yake ya pili na ya mwisho ya uongozi baada ya kuchaguliwa mwaka 2013 kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM), na kisha kutumia chama hicho kutetea kiti chake 2017.

You can share this post!

Mtoto aibwa mchana punde baada ya kuzaliwa

Wasichana 330,000 walipata mimba 2020 – Ripoti