Raila kukita kambi katika ngome ya Mudavadi

Raila kukita kambi katika ngome ya Mudavadi

NA DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga anatarajiwa kukita kambi katika Kaunti ya Vihiga wiki hii katika juhudi za kuvutia upande wake zaidi ya kura 300,000.

Bw Odinga kesho Jumatano ataongoza msururu wa mikutano katika Kaunti ya Vihiga inayochukuliwa kuwa ngome ya kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

Ziara hiyo ya Bw Odinga pia imezua tumbojoto miongoni mwa wawaniaji wanaotumia vyama tanzu vya muungano wa Azimio.

Ziara hiyo ni ya kwanza tangu Bw Odinga alipofanikiwa kumshawishi spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa Kenneth Marende kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana kupitia chama cha DAP-K.

Kiongozi wa Azimio ameahidi kumteua Bw Marende spika wa Seneti iwapo muungano huo utafanikiwa kuzoa idadi kubwa ya maseneta katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Kujiondoa kwa Bw Marende ilikuwa afueni kwa Gavana Wilber Ottichilo anayetetea wadhifa wake kupitia ODM.

Bw Marende na Dkt Ottichilo wote wanatoka katika kabila la Wanyore ambalo ni la pili kwa ukubwa baada ya Wamaragoli.

Seneta wa Vihiga George Khaniri pia anawania ugavana kupitia chama cha UDP ambacho kiko chini ya mwavuli wa Azimio.

Wawaniaji uwakilishi wa wanawake wanaotumia vyama tanzu vya Azimio ni Margaret Mbuni (Kanu), Kevina Shikutwa (Jubilee), Mary Amalemba (DAP-K), Violet Bagada (UDP) na Winnie Majani (ODM).

Wawaniaji wa useneta wa Azimio ni Eunice Vihenda (Wiper), Tyson Majani (Narc-K) na mbunge Maalumu Godfrey Osotsi (ODM).

Mshirikishi wa Azimio Kaunti ya Vihiga, Bw Osotsi alisema kuwa muungano huo haujajadili suala la kutaka baadhi ya wawaniaji wa Azimio wapokonywe tiketi.

Bw Khaniri aliwahakikishia wafuasi wake kuwa atakuwa debeni huku akipuuzilia mbali madai ambayo yamekuwa yakisambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba huenda akajitoa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana.

Bw Odinga anaelekea Vihiga siku chache baada ya Naibu wa Rais William Ruto, Bw Mudavadi na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kukita kambi katika eneo hilo kuwasihi wakazi kuunga mkono muungano wao wa Kenya Kwanza.

Bw Odinga atafanya mkutano katika ukumbi wa mikutano mjini Vihiga na kisha kuzuru maeneobunge yote matano ya kaunti hiyo.

Mkutano wa kampeni utaanzia katika uwanja wa michezo wa Hamisi na kuhutubia mikutano ya barabarani katika eneo la Cheptulu, Shamakhokho, Mudete, Chavakali, Mbale, Mahanga na kisha kuandaa mkutano mkubwa mjini Luanda.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Dkt Ruto asiwe wa kuwachenga wanawake,...

Gavana Lenku aitaka serikali kuu kutoa msaada wa chakula

T L