Habari MsetoSiasa

Raila kukutana na madiwani kumaliza mzozo wa uongozi

November 7th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

MADIWANI wa chama cha ODM katika Kaunti ya Nairobi kesho watakutana na kiongozi wao Raila Odinga ili kutatua mzozo kuhusu nafasi za uongozi wa walio wachache kwenye bunge la kaunti ambao umekuwa ukitokota kila mara.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema wawakilishi hao pia watakutana na kikosi kinachoratibu maswala ya chama katika kaunti ya Nairobi huku utata wa wanaofaa kutwaa nafasi hizo ukitishia kulemaza shughuli za chama hicho kwenye bunge la kaunti.

“Barua zinazowaarifu kuhusu mkutano huo zimetumwa kwa madiwani wote wa ODM. Utata kuhusu wanaofaa kushikilia vyeo hivyo utatatuliwa wiki hii ili kuleta kambi zote mbili pamoja,” akasema Bw Mbadi jana.

Madiwani wa ODM wamekuwa katika vita vikali dhidi ya viongozi wa wachache waliotekeleza mabadiliko kwenye uanachama wa kamati mbalimbali bila idhini ya uongozi wa chama chao.

Hatua hiyo ilipelekea Bw Mbadi kuwatema kiongozi wa wachache Elias Okumu na kiranja wa wachache Peter Imwatok baada ya wawili hao kukaidi agizo la chama na kutekeleza mabadiliko hayo yaliyozua pingamizi kutoka kwa madiwani.

Nafasi za wawili hao zilichukuliwa na diwani wa Highrise Kennedy Oyugi na mwenzake wa Lower Savanna Nicholas Ouma mtawalia kupitia barua aliyoandika Bw Mbadi kwa kaimu spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Chege Mwaura.

Hata hivyo Mkurugenzi mkuu wa ODM Oduor Ong’wen pia aliandikia Bw Chege akimtaka kupuuza barua ya Bw Mbadi ili uongozi wa chama hicho bungeni usalie jinsi ulivyokuwa zamani.

Kutokana na mtafaruku huo uliozidishwa na barua ya wawili hao, pande zote mbili zimekuwa zikidai zinaheshimu barua zinazowaunga mkono kuwa ofisini hali ambayo imechangia kuitishwa kwa mkutano wa kesho na kinara wao.