HabariSiasa

Raila kupimwa makali tena

August 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

UCHAGUZI mdogo katika eneobunge la Kibra, Kaunti ya Nairobi umetoa nafasi kwa Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kujipima nguvu tena baada ya ushawishi wake kisiasa kuonekana kudidimia tangu handisheki.

Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha Ken Okoth mnamo Julai 26 kutoka na saratani.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatatu ilitangaza uchaguzi huo mdogo utafanywa Novemba 7 na hivyo kufungua rasmi ushindani wake.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, alisema vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki katika kinyang’anyiro hicho vinahitajika kufanya mchujo kuteu wagombeaji wao Septemba 9 na Septemba 10 kabla ya kampeni kuanza rasmi na kukamilika Novemba 4.

Tangu Machi 9, 2018 alipoweka mwafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga ameshindwa kushawishi wapigakura kuunga mkono wagombeaji wa ODM kwenye chaguzi tatu ndogo za ubunge zilizofanywa kufikia sasa.

Katika chaguzi ndogo zilizofanyika Aprili 4 mwaka huu katika maeneo bunge ya Embakasi Kusini na Ugenya, Bw Odinga aliaibishwa vibaya baada ya wagombeaji wa ODM kuangushwa.

Katika eneo bunge la Ugenya, ambako ni mojawapo ya ngome zake kuu za kisiasa, David Ochieng’ aliyewania kwa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) alimshinda mgombezi wa ODM, Chris Karan.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, Julius Mawathe wa chama cha Wiper alimzima Irshad Sumra wa ODM.

Katika uchaguzi mdogo wa Wajir Magharibi, ODM ilijiondoa mapema baada ya kushindwa kuwavutia wapiga kura wa eneo hilo, na aliyetarajiwa kuwa mgombeaji wao, Prof Mohamed Yusuf Elmi akajiondoa.

Kando na chaguzi hizi za ubunge, ODM pia iliponea chupuchupu katika uchaguzi mdogo wa useneta Migori ambapo mgombeaji ODM, Ochilo Ayacko alimshinda mwanasiasa chipukizi Eddy Oketch wa Federal Party of Kenya pembamba.

Kufikia sasa takriban watu saba wameonyesha nia ya kuwania kiti Kibra ambacho kimewahi kushikiliwa na Bw Odinga kuanzia 1992 hadi 2013, lilipokuwa pamoja na eneo bunge la sasa la Langata.

Wao ni pamoja na kakake marehemu Okoth, Imran Okoth, Katiba Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, kiongozi wa vijana eneo la Kibra Benson Musungu, Bw Sumra, aliyekuwa mshauri wa Odinga Eliud Owalo, wanawe Bw Odinga Rosemary na Winnie Odinga na mjane wa marehemu Okoth, Monica.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anasema Bw Odinga atahitajika kutumia funzo alilopata katika chaguzi tatu zilizopita kwa kuhakikisha kuwa mchujo wa ODM unaendeshwa kwa haki na uwazi.

“Mchujo utakaoendeshwa kwa haki na uwazi bila mapendeleo ndio utaiwezesha ODM kuhifadhi kiti cha Kibra kwa urahisi. Lakini Odinga akirudia kosa lililofanyika Migori, Ugenya na Embakasi Magharibi la kupeana tiketi ya moja kwa moja kwa mgombeaji anayependelewa, basi atashangazwa tena katika ngome yake ya Kibra,” akasema.

Uongozi wa ODM unakutana wiki hii kujadili mfumo utakaotumiwa kuteua atakayepeperusha bendera yake Kibra.