HabariSiasa

Raila kupumzika nyumbani kwake kwa wiki tatu

July 19th, 2020 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG

WAFUASI na mahasimu wa kisiasa wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, watalazimika kusubiri kwa muda zaidi kabla arejelee shughuli zake za kawaida.

Baada ya kurudi nchini kisiri kutoka kwa matibabu Dubai Jumapili iliyopita, sasa imebainika Bw Odinga anatakikana kupumzika kwa siku 21.

Hii ni kumaanisha kuwa, Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) linatarajiwa kuchelewa zaidi kuwasilisha ripoti yake, ambayo inasubiriwa kwa hamu na wanaoegemea upande wa handisheki yake na Rais Uhuru Kenyatta sawa na wanaopinga.

Mapumziko hayo yanatokana na kuwa Bw Odinga alifanyiwa upasuaji wa mgongo katika hospitali iliyo Dubai.Aliporudi nchini Jumapili iliyopita, ilitangazwa atahitaji kupumzika kwanza lakini haikujulikana kwa muda gani.

Jopo la BBI linaloongozwa na Seneta wa Garissa, Bw Yusuf Haji, lilikamilisha kazi yake lakini lingali linasubiri kupewa siku ya kuwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.Wawili hao ndio ndio waasisi wa mchakato huo unaolenga kurekebisha katiba.

Mnamo Alhamisi, Bw Odinga alikutana kisiri na viongozi kadhaa wa kutoka eneo la magharibi walioongozwa na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya nyumbani kwake Karen, Kaunti ya Nairobi.

Ni katika mkutano huo ambapo alifichua kwamba hatahusika katika siasa wala shughuli nyingine nzito kwa angalau siku 21.

Kando na Bw Oparanya, viongozi wengine waliokutana na balozi huyo wa miundomsingi anayewakilisha Muungano wa Afrika (AU) ni Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na Mbunge Maalumu Godfrey Osotsi.

Imebainika kuwa, mengi yaliyojadiliwa katika mkutano huo yalihusu afya ya Bw Odinga, wala si siasa.

‘Wasiwasi wetu ulikuwa kuhusu hali yake ya afya, na ninaweza kuthibitisha anaendelea vyema. Anaweza kusimama peke yake na ana nguvu,’ akasema mmoja wa waliofahamu kuhusu mkutano huo.

Waliokuwepo hawakuruhusiwa kumpiga Bw Odinga picha na wale waliopiga picha waliagizwa kutozisambaza kwa umma.

‘Alikuwa mwenye furaha akatuambia upasuaji aliofanyiwa katika sehemu ya chini ya mgongo wake ulifanikiwa,’ Taifa Jumapili ikaelezwa.

Bw Oparanya alisema kuwa, alimtembelea Bw Odinga kwa vile yeye ndiye naibu kiongozi wa ODM.

‘Anapumzika kwa siku 21 alivyoagizwa na madaktari kwa hivyo hatungejadili siasa, na wala BBI haikuwa katika ajenda yangu. Nilikuwa nimeenda kumtembelea kwa vile alirudi nchini kutoka kwa matibabu,’ akasema mwenyekiti huyo wa Baraza la Magavana.

Aliongeza: ‘Alizungumzia sana upasuaji wake kwa hivyo tunataka kusubiri apone kabisa ndipo tuzungumzie siasa. Ni lazima akamilishe siku 21 za mapumziko na hakuna shughuli za kisiasa tutakazofanya kwa muda huo.’

Bw Odinga alirudi nchini kimya kimya Jumapili iliyopita, kwa ndege ya kifahari aina ya Airbus A318.Awali, Bw Haji alikuwa ameambia Taifa Jumapili kwamba watawasilisha ripoti ya BBI wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga watakapokuwa tayari.