HabariSiasa

RAILA: Kwa nini simpendi Ruto

August 2nd, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM Raila Odinga hatimaye amefichua kiini cha uhasama baina ya chama chake na Naibu wa Rais William Ruto.

Bw Odinga alisema naibu wa rais anajihusisha na kampeni za mapema ambazo ni kinyume na muafaka aliotia saini na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Mei 9.

“Kampeni za 2022 si miongoni mwa masuala tuliyoafikiana na Rais Kenyatta. Mimi na Rais Kenyatta tuliafikiana kutatua dosari zilizoshuhudiwa katika uchaguzi wa 2017 kwanza kabla ya kuanza kuzungumzia uchaguzi wa 2022,” akasema Bw Odinga katika mahojiano na runinga ya humu nchini.

“Hatutaki kuanza kampeni za 2022 kabla ya kushughulikia mzozo wa uchaguzi 2017. Hiyo ndiyo sababu chama cha ODM kimepiga marufuku viongozi wake kujihusisha na siasa za uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Odinga.

Bw Odinga aliwataka wabunge wa Pwani; Aisha Jumwa (Malindi) na Suleiman Dori (Msambweni), ambao tayari wametangaza kuunga mkono Bw Ruto kuwania urais 2022, kujiuzulu kutoka chama cha ODM na kurejea kwa wapiga kura ili wachaguliwe kwa kutumia chama tofauti.

Chama cha ODM kimewapa Bi Jumwa na Bw Dori makataa ya siku saba kujitetea la sivyo watimuliwe chamani.

“Nimeagiza viongozi wa ODM kumkaribisha Naibu wa Rais Ruto anapozuru maeneobunge yao kwa ajili ya maendeleo. Lakini wametakiwa kujiepusha na siasa za 2022,” akasema Bw Odinga.

“Mbona wampigie debe mwaniaji wa chama kingine ilhali muungano wa NASA au vyama tanzu: ODM, Ford-Kenya, Wiper na ANC havijatangaza ikiwa vitawasilisha mwaniaji wa urais 2022 au la?” akauliza Bw Odinga. Waziri Mkuu aliyeonekana kuwa mwangalifu na matamshi yake, alikataa kufichua ikiwa ana azma ya kuwania urais 2022 au la.

Alikanusha madai kuwa alimshauri Rais Uhuru Kenyatta kumtenga Bw Ruto katika mazungumzo yaliyowafanya kukubaliana kufanya kazi pamoja na hatimaye kusalimiana mnamo Machi 9.

“Mazungumzo yalikuwa baina ya watu wawili waliokuwa wameapishwa kuwa marais. Sijui ikiwa Rais Kenyatta alishauriana na Bw Ruto wakati wa mazungumzo. Lakini ninachojua ni kwamba, mazungumzo yalikuwa ya watu wawili na hakuna mtu wa tatu aliyehusishwa,” akasema.

Bw Odinga alisisitiza kuwa bado angali kiongozi wa Upinzani na hajajiunga na serikali.

Alisema lengo kuu la muafaka baina yake na Rais Kenyatta ni kuunganisha Wakenya na kushughulikia masuala nyeti kama vile ufisadi, dhuluma za kihistoria, ukabila, ukosefu wa ajira, ugatuzi kati ya masuala mengineyo.

“Mimi siko serikalini, kama ningekuwa serikalini basi ningekuwa na cheo. Mimi niko nje ya serikali na ningali kiongozi wa NASA na chama cha ODM,” akasema.

Bw Odinga pia alijitetea kuwa anaendelea kupigana na ufisadi serikalini licha ya kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta.

“Zamani nilikuwa nahutubia vyombo vya habari sakata ya ufisadi ilipojitokeza serikalini. Upande wa serikali ulikuwa ukikimbilia kukanusha madai yangu. Lakini sasa ninampigia Rais Kenyatta simu moja kwa moja na sakata hiyo inashughulikiwa,” akasema.