Siasa

Raila kwa Ruto: Umevuka mstari mwekundu

January 3rd, 2024 1 min read

FARHIYA HUSSEIN Na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amemuambia Rais William Ruto kwamba amevuka mstari mwekundu kwa kuishambulia idara ya Mahakama akimuonya Wakenya hawataruhusu aitumbukize nchi kwa udikteta.

Bw Odinga akiwahutubia wanahabari jijini Mombasa, amesema ana kila mikakati ya kuikabili serikali hadi itii sheria na pia kupunguza gharama ya maisha.

“Mnamo Januari 2, 2023, Mheshimiwa (Rais)¬†William Ruto alijitokeza kwa ujasiri na makali akionyesha udikteta uliovuka mipaka,” amesema Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa ODM aliye pia kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya, amesema vitisho vya Rais Ruto dhidi ya Mahakama vinaonyesha kwamba ni “kiongozi aliye na machungu kwa kukodolea macho ukweli kwamba amefeli”.

“Vitisho vya serikali ya Kenya Kwanza ni dhihirisho tosha kuwa ni kisingizio cha kukwepa ukweli wa mambo kwa ‘ground’, haswa changamoto za kijamii na kiuchumi ambazo imewaelekezea raia,” amesema Bw Odinga.

Kiongozi huyo ambaye anadai alipokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, amesema kwa Rais Ruto kuishambulia mahakama, ni wazi kwamba analemaza zaidi misingi ya demokrasia.

“Hivyo ni muhimu tumuambie Ruto wazi kwamba amevuka mstari mwekundu. Bila shaka Wakenya wanakumbuka kwamba wakati Mahakama ya Upeo ilipotupa kesi yetu ya kupinga matokeo ya kura za urais mwaka 2022, tulisema tunapinga vikali, lakini tunakubali ili kudumisha sifa ya uzingatiaji wa sheria, demokrasia, mshikamano na uponyaji wa taifa,” akasema Bw Odinga.