Raila: Mambo yako hivi…

Raila: Mambo yako hivi…

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa muungano wa Azimio Raila Odinga amefafanua wafuasi wake hawatavamia Ikulu ya Nairobi Jumatatu jinsi ilivyodhaniwa ila ni wachache watatumwa huko kuwasilisha taarifa yenye malalamishi yao.

Akiongea kwenye mahojiano katika runinga za Citizen TV na TV47, Jumamosi usiku Bw Odinga alikariri kuwa maandamano yao jijini Nairobi, Jumatatu, Machi 20, 2023 yatakuwa ya amani.

“Wafuasi wetu watafanya maandamano ya amani jijini Nairobi Jumatatu jinsi tulivyopanga. Kisha watu wawili au watatu kati yetu wataelekea Ikulu kuwasilisha taarifa ya malalamishi kwa Rais William Ruto. Tungeenda katika Afisi za Rais zilizoko jumba la Harambee lakini siku hizi Ruto huwa hafanyi kazi kule,” akaeleza.

“Aidha, kwa wafuasi wetu katika maeneo mengine ya nchini ambao hawataweza kufika Nairobi, tunawahimiza kufanya maandamano kisha kuwasilisha taarifa zao za malalamishi katika afisi za Makamishna wa Kaunti,” Bw Odinga akaongeza.

Habari zimekuwa zikisambazwa mitandaoni kuashirikia kuwa kilele cha maandamano ya Nairobi itakuwa ni “uvamizi wa Ikulu ya Rais”.

Ni baada ya kuenea kwa habari hizo ambapo serikali kuweka ulinzi mkali katika barabara za kuelekea katika Ikulu ya Nairobi na ile ya Kisumu.

Bw Odinga hata hivyo alisisitiza kuwa Azimio hailengi kufanya maandamano kwa “sisi ni watu wanaoheshimu sheria”.

“Sisi ni watu wanaoheshimu sheria.. hii ndio maana kiongozi wetu Wycliffe Oparanya alimwandikia Inspekta Jenerali wa polisi akimwarifu kuwa tutafanya mkutano na maandamano,” Bw Odinga akasema.

“Yatakuwa ni maandamano ya amani na wafuasi wetu watapeleka memoranda katika afisi mbalimbali za serikali. Hapa Nairobi tutapeleka memoranda kwa Rais. Ikiwa atakuwa katika Jumba la Harambee, tutapeleka taarifa yetu huko. Ikiwa atakuwa katika Ikulu tutatuma watu kule, sio umati,” akaeleza.

Alipoulizwa ikiwa yeye ni miongoni mwa wale watakaotumwa Ikulu kupeleka taarifa ya malalamishi yao, Bw Odinga alisema kamati ya Azimio ndio itateua watakaowasilisha hati hiyo.

“Watu wachache watateuliwa kupeleka malalamishi yetu kwa Rais. Sijui ikiwa nitakuwa miongoni mwa watu wataoteuliwa na wanachama kupeleka taarifa hiyo,” akakariri.

Bw Odinga alisema hamna makosa yoyote kwa wafuasi wake kwenda Ikulu, ambayo ni eneo lenye ulinzi mkali.

“Kikatiba Ikulu ni makazi ya Rais wa Jamhuri na ni afisi ya umma na kila Mkenya anayo haki ya kufika huko,” akasema.

Hata hivyo, Bw Odinga alisema ikiwa wawakilishi wa Azimio watazuiwa kuingia Ikulu wataachna taarifa yao kwa walinzia katika lango kuu la Ikulu.

Bw Odinga alisema kuwa maandamano yao yataendelea hata baada ya Jumatatu “kwa njia mbalimbali hadi siku ambayo serikali itatimiza matakwa yetu.”

  • Tags

You can share this post!

Wandani wa Ruto walia kuachwa nje ya teuzi mbalimbali...

Vuguvugu la wahubiri 500 lataka Raila asitishe maandamano

T L