Habari

Raila, Mudavadi watofautiana kuhusu kura ya maamuzi

August 17th, 2019 2 min read

Na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga na kinara wa Amani National Congress (ANC) Wycliffe Musalia Mudavadi, wametofautiana Jumamosi kuhusu maandalizi ya kura ya maamuzi nchini.

Bw Odinga aliwarai Wakenya kuwa na subira Jopo la Maridhiano (BBI) linapoendelea kuandaa ripoti yake, ambayo huenda likapendekeza mageuzi kadhaa ya kikatiba.

Lakini kauli hiyo ilikinzana na ile ya Bw Mudavadi ambaye alionya kwamba, Katiba haipaswi kugeuzwa kila baada ya uchaguzi.

Kauli za viongozi hao zinajiri wakati hali ya taharuki inaendelea kuwepo nchini baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupitisha Mswada wa Punguza Mizigo, ambao pia huenda ukaifanya nchi kushiriki kura ya maamuzi. Mswada huo tayari ushawasilishwa kwa mabunge yote 47 ya kaunti kujadiliwa.

Wawili hao walikuwa wakihutubu jana katika eneo la Lusengeli, Sabatia, Kaunti ya Vihiga, kwenye mazishi ya Dkt Sobbie Mulindi, aliyehudumu kama mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi na Naibu Mkurugenzi katika Baraza la Kitaifa la Kukabiliana na Ukimwi (NACC) kati ya 2008 na 2014. Pia, aliwahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya AFC Leopards.

Bw Mudavadi alifika kwenye mazishi hayo baada ya Bw Odinga kuwahutubia waombolezaji na kuondoka, ambapo jumbe zao zilionekana kutofautiana.

Bw Odinga alipuuzilia mbali Mswada wa Punguza Mizigo, akisema wanajopo wa BBI walizunguka kote nchini na kukusanya maoni ya Wakenya kutoka kaunti zote 47, ambapo sasa inaandaa ripoti yake. Alisema kuwa BBI inalenga kuwaunganisha Wakenya.

“Tunataka kuondoa ukabila kwa kukataa kugawanyika kwa misingi ya tofauti zetu.

Tunataka kurejesha uwajibikaji katika mfumo wetu wa uchaguzi kwa kuhakikisha uwazi. Tunalenga kukabiliana na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma,” akasema.

Akaongeza: “Tuliwaahidi kwamba tu njiani kuelekea Kanani. Kupitia BBI, tutakabili changamoto kama ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, hali ambayo itatusaidia kumaliza umaskini na ukosefu wa usalama.”

Kila wakati

Kwa upande wake, Bw Mudavadi alisema ni hatari kwa nchi kuifanyia mageuzi Katiba kila wakati.

Hata hivyo, alisema ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi, basi mageuzi hayo hayapaswi kuwafaidi wanasiasa pekee.

“Tulikuwa na Katiba kutoka vikao vya Lancaster, ambayo ilibadilishwa. Tulipata Katiba mpya mnamo 2010, na tayari kuna juhudi za kuifanyia mageuzi. Ikiwa lazima tufanye kura ya maamuzi, tunapaswa kuhakikisha kuwa tunazingatia maoni ya wananchi. Changamoto kubwa zaidi zinazotuandama ni ufisadi, ukosefu wa ajira na umaskini,” akasema.

Hata hivyo, wawili hao walikubaliana kwamba kuna haja ya mageuzi kuhusu mfumo wa uchaguzi nchini.