HabariSiasa

Raila na Ruto waonywa dhidi ya kuibua uhasama

October 2nd, 2018 2 min read

BENSON MATHEKA na VICTOR OTIENO

VIONGOZI wa makanisa nchini wameonya kuwa malumbano kati ya wanasiasa yanaweza kusababisha hali ya taharuki nchini iwapo yataendelea.

Kwenye taarifa, viongozi wa makanisa eneo la Nyanza walisema wameshangazwa na madai ya baadhi ya wanasiasa kwamba kuna matapeli waliojiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma wakisema matamshi hayo ni hatari kwa amani nchini.

Onyo la viongozi hao linajiri huku Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa NASA Raila Odinga wakiendelea kurushiana lawama hadharani baada ya Bw Ruto kudai Raila anatumia utapeli kugawanya viongozi wa Jubilee.

Akiongea akiwa Kilifi mwishoni mwa wiki, Bw Ruto alimlaumu Raila kwa kupanga njama ya kutimuliwa kwake katika Jubilee.

“Kama mnataka kunifukuza Jubilee mlivyonifukuza ODM, ninawaambia sitakubali,” alisema Bw Ruto.

Matamshi hayp yaliwakera wafuasi wa Bw Odinga ambao wamedai kuwa Naibu Rais anataka kumtumia Raila kama kisingizio cha kuhama Jubilee.

Kulingana na viongozi wa makanisa eneo la Nyanza, matamshi hayo ni hatari kwa amani iliyoshuhudiwa nchini tangu Bw Odinga na Rais Kenyatta walipotangaza muafaka wao.

“Tunataka kusema waziwazi kwamba tunashangazwa na matamshi ya baadhi ya wanasiasa wanaodai kuwa kuna matapeli waliojiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma. Matamshi kama hayo yanalenga kugawanya Wakenya na sio kuwaunganisha na hayafai kuruhusiwa kamwe,” alisema Askofu Washington Ogonyo Ngede aliyezungumza kwa niaba ya viongozi hao.

Muafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga uliopatikana mnamo Machi 9 mwaka huu, ulituliza joto la kisiasa nchini baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana uliojaa uhasama.

Viongozi hao walimtaja Bw Odinga kama kiongozi wa hadhi kuu, mzalendo anayependa Kenya na kuwataka wanaotoa matamshi ya kumdhalilisha kama ya Naibu Rais, kukoma.

“Bw Odinga anafaa kuheshimiwa kama mwanasiasa mashuhuri katika nchi hii kwa sababu ya kupigania demokrasia na utawala bora,” ilisema taarifa ya viongozi hao iliyosomwa na Askofu Ngede.

Waliwataka Wakenya kukataa ushawishi wa wanasiasa wanaotaka kuwatumia kutimiza maslahi yao ya kibinafsi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Canon Peter Karanja alisema ni kawaida ya wanasiasa kurushiana lawama kila wakati.

“Wakenya hawafai kushtushwa na matamshi ya wanasiasa. Malumbano ni sehemu ya maisha yao na wanajuana kwa vilemba. Wanalaumiana hadharani huku wakikutana faraghani na baada ya muda wanasalimiana tunashangaa,” alisema Canon Karanja akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu

Hata hivyo, alisema kanisa halitanyamaza ikiwa wanasiasa hao watavuka mipaka.

“Ikiwa hali itakuwa mbaya zaidi, kanisa halitanyamaza. Kwa sasa hali ya kisiasa ya Kenya ni shwari lakini uchumi umedorora,” alisema Canon Karanja.

Aliwataka Wakenya kuombea nchi na viongozi wao na kutokubali kugawanywa na wanasiasa kwa misingi yoyote ile.