Siasa

Raila na Ruto wataifaa Kenya?

September 15th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga hawana uwezo wa kuboresha maisha ya Wakenya iwapo yeyote kati yao atachaguliwa rais 2022.

Wachanganuzi wa uchumi, jamii na siasa wanasema wawili hao wataendeleza mtindo wa viongozi kulinda maslahi ya tabaka la wanasiasa na matajiri huku raia wakiendelea kuumia.

Wakili Lempaa Suyianka anasema hakuna chochote wawili hao watafaa Kenya nacho kwa sababu wanaongozwa na falsafa ya kulinda tabaka la juu na mali yao.

Wadadisi wanahoji kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga wamejenga siasa zao kwenye misingi ya kikabila na kimaeneo pamoja na kutoa ahadi, lakini hawana mbinu mahsusi za kuimarisha maisha ya wananchi wa kawaida.

Bw Odinga, ambaye alianza siasa kama mtetezi shupavu wa demokrasia, amebadilika pakubwa na imani aliyokuwa amewapa Wakenya wengi kuwa uongozi wake unaweza kuboresha maisha yao inazidi kuyeyuka.

Alidhihirisha haya alipokuwa katika serikali ya muungano akiwa waziri mkuu, ambapo aliwasahau waliomchagua huku akiteua jamaa na washirika wake serikalini.

Vile vile, alipoingia handisheki na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018 aliwasahau wafuasi wake na kuunga mkono serikali inayoendelea kulaumiwa kwa ufisadi, madeni na kuongezeka kwa umaskini.

Kwa sasa Bw Odinga yumo mstari wa mbele kuhimiza marekebisho ya kikatiba kwa lengo la kujinufaisha binafsi.

Wadadisi wanasema mienendo hii ya Bw Odinga imeonyesha kuwa hana msimamo, sera wala ajenda thabiti kuhusu Kenya.

“Kwa kuacha ajenda za upinzani na kuunga mkono serikali aliyokuwa akikosoa kwa utawala mbaya na ufisadi, Bw Odinga ameonyesha kuwa hawezi kuaminiwa kuokoa nchi hii jinsi Wakenya walivyofikiria alipokuwa akitetea demokrasia na utawala bora. Ameonyesha kuwa akiingia mamlakani, serikali yake haitakuwa tofauti na anayounga mkono kwa sasa,” asema mtaalamu wa utawala bora Silas Okumu.

Kulingana na Bw Okumu, Wakenya hawafai kutarajia wanasiasa wakuu wawaokoe kutoka kwa matatizo yanayowakabili.

“Kenya inaweza kubadilika tu iwapo wataalamu wa kila sekta wataungana kwa ajili ya Kenya na wakatae kutumiwa na wanasiasa. Ruto na Raila ni kitu kimoja,” asema Bw Okumu.

Anasema kwa kuunga mkono serikali ya Jubilee, Bw Odinga ameonyesha kwamba alikuwa akijifanya alipokuwa akiilaumu.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba Raila akiwa rais atalinda maslahi ya familia na washirika wake wa kisiasa waliotajwa katika ufisadi. Amebadilika sana. Huyu sio yule Raila ambaye Wakenya walidhani akiwa rais angeokoa nchi kutokana na utawala mbaya,” asema.

Dkt Ruto na Bw Odinga walikutana katika serikali ya Mzee Daniel Moi wakiwa mawaziri mnamo 1997.

“Ruto, Raila na hata Uhuru walijifunza masuala ya utawala wakiwa katika serikali ya Moi, na hivyo uongozi wao hauwezi kuwa tofauti na wa Kanu,” asema Bw Okumu.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya uchumi Rita Nyokabi, Dkt Ruto na Odinga hawana ajenda thabiti zinazoweza kuboresha maisha ya Wakenya.

“Dkt Ruto anafanya kampeni yake kwa kutaja Wakenya 17 milioni wanaokabiliwa na umaskini mkubwa, na vijana milioni sita wasio na kazi. Lakini anachofanya ni kuwatumia kupiga vita wapinzani wake bila sera thabiti ya kuimarisha maisha yao. Hii ni licha yake kuwa naibu rais kwa miaka minane,” asema Bi Nyokabi.

“Bw Odinga naye amewaacha vijana na kuungana na matajiri kutaka katiba irekebishwe kulinda maslahi yao. Kilicho muhimu kwake wakati huu ni kubuni nafasi zaidi serikalini ambazo zitatwaliwa na wanasiasa wenye majina makubwa ili waendelee kufyoza Wakenya,” asema Bi Nyokabi.

Mtaalamu wa masuala ya kikatiba wakili Waikwa Wanyoike, anasema Wakenya wamepotoshwa kwa taswira kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta anaweza kuwa tu Bw Odinga ama Dkt Ruto.

“Kuchagua mmoja wa wawili hao ni kuchagua wanaofanya watu watumwa wa kisaikolojia ili wapate nafasi ya kupora nchi,” asema Bw Wanyoike.

Anasema Wakenya wanahitaji viongozi watakaohakikisha vijana wakisoma wanapata kazi, wakulima wanalindwa na wafanyabiashara wana mazingira bora ya kuhudumu.

Wadadisi hawa wanasema huku Dkt Ruto akihusishwa na madai ya ufisadi, Bw Odinga anazingirwa na wanasiasa na washirika ambao wanataka aingie mamlakani ili wapate nafasi ya kujinufaisha kwa mali ya umma, hivyo hawatakuwa na uwezo wa kumaliza ufisadi

Bw Ouma anasema Dkt Ruto hawezi kujitenga na maovu ya Jubilee ambayo Bw Odinga kwa sasa anaunga mkono kupitia handisheki, ukiwemo mzigo wa madeni na ufisadi.