Siasa

Raila na Wanjigi: Urafiki wa presha inapanda, presha inashuka

January 10th, 2024 2 min read

NA NDUBI MOTURI

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga mnamo Jumanne alikutana na kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi, siku chache baada ya wawili hao kuonya kuitisha maandamano ili kuishinikiza serikali ipunguze gharama ya maisha.

Bw Odinga na Bw Wanjigi walikutana katika mkahawa mmoja jijini Nairobi kwa muda wa zaidi ya saa mbili kabla kila mmoja kwenda zake.

Walidinda kuongea na wanahabari ambao walikuwa wamepiga kambi nje ya hoteli hiyo.

Hata hivyo, duru ziliambia Taifa Leo kwamba mazungumzo kati ya wanasiasa hao wawili yalihusu gharama ya maisha na viwango vya juu vya ushuru vilivyowekwa na serikali ya Kenya Kwanza.

Hata hivyo, haikujulikana waziwazi ikiwa Mbw Odinga na Wanjigi walikubaliana kuhusu namna ya kuisukuma serikali kushughulikia masuala hayo mawili.

Mnamo Desemba 30, 2023, Bw Odinga aliitaka serikali kufanyia mageuzi Sheria ya Fedha ya 2023 ili kuondoa ushuru wa nyumba la sivyo ahimize wafuasi wake kurejelea maandamano.

“Gharama ya maisha ni juu zaidi. Tuliwaambia wasiongeze lakini wameendelea kufanya kinyume. Sheria ya Fedha sharti ifanyiwe mageuzi ili kuondoa ushuru mwingi unazoumiza Wakenya kama vile wa nyumba. Wasipofanya hivyo, tutarejea barabarani,” Bw Odinga alisema alipohudhuria hafla moja ya kitamaduni katika eneo la Usenge, eneobunge la Bondo katika Kaunti ya Siaya.

Kwa upande wake Bw Wanjigi alipohudhuria hafla moja ya mazishi eneobunge la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, pia alisema kuwa Kenya Kwanza inafaa kuibua mbinu mpya za kupunguza gharama ya maisha.

“Wasipofanya hivyo, nakubaliana na Bw Odinga kuwa njia ya maandamano ndio inapasa kutumika kuilazimisha kuitikia vilio vya Wakenya. Hauwezi kuamka kila siku na kuongeza ushuru. Tumekupa makataa ya miezi mitatu upunguze ushuru la sivyo tutumie nguvu za wananchi,” Bw Wanjigi akasema.

Mkutano wa Jumanne ulikuwa wa kwanza kwa Bw Odinga na kiongozi huyo wa Safina kuufanya katika siku za hivi punde.

Bw Wanjigi alijaribu kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 lakini akazuiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kukosa kutimiza matakwa ya kisheria.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mfanyabiashara tajika, alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais baada ya kukosana na Bw Odinga na kugura ODM mapema mwaka huo wa 2022.

Hii ni baada ya Bw Wanjigi kuzuiwa kung’ang’ania tiketi ya kuwania urais kwa tiketi ya ODM wakati wa Kongamano la Wajumbe wa chama hicho (NDC) lililofanyika katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi.

Hii ina maana urafiki wa wawili hawa ni wa mara presha inapanda, presha inashuka.

Ingawa hivyo, wachambuzi husema kwamba kwa siasa, hakuna uadui wa milele.