Habari MsetoSiasa

Raila ni mkono gamu, makanisa ya Nyanza yasema

April 23rd, 2019 2 min read

Na RUSHDIE OUDIA

BAADHI ya viongozi wa makanisa eneo la Nyanza wamemkashifu kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga kwa kuwakataza kupokea pesa za watu ambao maadili yao yanatiliwa shaka, wakisema yeye mwenyewe ni mkono gamu.

Mwishoni mwa wiki, Bw Odinga alidai kuwa makanisa yanatumiwa vibaya na viongozi wa kisiasa wasio na maadili, kwa kupewa pesa zisizojulikana chanzo chake.

Kiongozi wa kanisa la Episcopal Askofu Joshua Koyo na mwenzake wa kanisa la Anglikana nchini (ACK) dayosisi ya Maseno, Askofu Charles Onginjo, walimtaka Bw Odinga ayaheshimu makanisa, na kuacha kutoa maneno ya kuyachafulia sifa.

Mnamo Jumamosi, Bw Odinga alisema kiwango cha pesa ambazo zinapelekwa makanisani kila wikendi na watu ambao maadili yao ni ya kutiliwa shaka ni kikubwa. Aliyalaumu makanisa kwa kuwapokea watu na michango bila kujali inakotoka.

Alidai pesa zinazofaa kuwa za kutekeleza maendeleo zinaibiwa na kutumika katika michango makanisani.

“Hizi ni pesa ambazo zinafaa kutumika kugharamia matibabu kwa Wakenya, kulipa mishahara ya walimu, kutengeneza barabara, shule na hospitali. Hawa ni maadui kwa Wakenya,” Bw Odinga akasema jijini Kisumu.

Akimrejelea Naibu Rais William Ruto, Bw Odinga alimtaka kueleza anakopata pesa, akitaja hali yake ya kuendelea kuchanga pesa katika harambee bila kueleza anakozipata kuwa ukosefu wa maadili.

“Anatembea kutoka kanisa hadi jingine kila wikendi kuchanga pesa huku waumini wakimpigia makofi, wala hakuna anayeuliza mahali anakotoa pesa. Tunajua mshahara wake ni Sh1 milioni kila mwezi, lakini anatoa hadi Sh100 milioni kwa mwezi,” akasema Bw Odinga.

Lakini akimjibu, Askofu Koyo alimtaka Bw Odinga kukoma kulaumu makanisa kuhusiana na serikali kufeli katika vita dhidi ya ufisadi.

Bw Koyo alisema makanisa yana miradi ya maendeleo ambayo yanaendeleza, na ambayo inahitaji msaada wa kifedha kutoka kwa wahisani. Askofu huyo alisema Bw Odinga huwa hatoi msaada kwa kanisa na ndiposa anakosoa wale wanaotoa.

“Tuna njia za kuzungumza kuhusu ufisadi lakini hatuna nguvu za kukamata washukiwa na kuwapeleka kortini. Hivyo, hatufai kulaumiwa,” akasema Bw Koyo.

Aidha, alisema kuwa vita dhidi ya ufisadi vitafanikiwa tu endapo wale wanaoviendesha watajitolea bila azima nyingine.

Askofu Ogonjo naye alishangaa sababu ya baadhi ya watu kuhisi wao wanafaa sana kupewa nafasi kanisani, ilhali wengine wakipewa wanazua ubishi.

“Tukisema hatutaki wanasiasa kanisani, iwe kwa kila mtu. Ilivyo sasa, haijulikani nani anafaa kupokelewa na nani hafai,” akasema Bw Oginjo.

Lakini askofu huyo alikiri kuwa makanisa yamekuwa yakiwapa wanasiasa hadhi isiyofaa madhabahuni, hali ambayo sasa inaonekana kama kwamba wanapendelewa. Alizungumza baada ya ibada katika eneo la Dago, Kaunti ya Kisumu.