Raila njiapanda Pwani ikijitafutia ‘mkombozi’ mpya

Raila njiapanda Pwani ikijitafutia ‘mkombozi’ mpya

Na WANDERI KAMAU

IMEIBUKA kuwa huenda uasi wa kisiasa unaomkumba kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, katika ukanda wa Pwani ni mwiba wa kujidunga mwenyewe.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Odinga amekuwa kwenye majibizano makali na viongozi kadhaa wa Pwani, kuhusu hatua yake kupinga pendekezo lao kubuni chama kimoja cha kisiasa.

Mnamo Jumatano, Bw Odinga alikosolewa vikali na Gavana Amason Kingi wa Kilifi kwa kupinga hilo, akitaja msimamo wa kiongozi huyo kama “kejeli” kwa wenyeji wa Pwani.

Bw Odinga pia amejipata kwenye njiapanda kisiasa, kuhusu mustakabali wa uhusiano wake wa karibu na Gavana Hassan Joho wa Mombasa, kufuatia tangazo la Bw Joho kuwa atawania urais.

Wawili hao wamekuwa washirika wa karibu wa Bw Odinga, ikizingatiwa walichaguliwa kwa tiketi ya ODM.Mwezi uliopita, Bodi ya Kitaifa ya Chaguzi ya ODM (NEB), iliahirisha ghafla tarehe ya wale wanaotaka kuwasilisha maombi yao kuwania urais kwa tiketi hiyo, hatua ambayo ilipokelewa kwa hisia mseto na baadhi ya wafuasi wa Bw Joho.

Majibizano hayo yakiendelea, wadadisi wa siasa za Pwani wanasema sababu kuu ya uasi wa kisiasa dhidi ya Bw Odinga umechangiwa na kosa lake kutosoma mabadiliko ya nyakati, mchipuko wa kizazi kipya, wenyeji kupoteza imani naye kama ‘mtetezi’ wao na kimya chake kuhusu matatizo ya kiuchumi yanayowakabili.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, Prof Halimu Shauri, ambaye ni mdadisi wa siasa za Pwani, alisema Bw Odinga amenyamazia masaibu yanayowaathiri Wapwani kama kudorora kwa kilimo cha mazao kama korosho na matatizo yaliyoletwa na Reli ya Kisasa (SGR).

“Tangu 2007, Bw Odinga amekuwa na ushawishi mkubwa kisiasa Pwani, kwani walimwona kama mtetezi wa maslahi yao. Sababu kuu ni kuwa eneo hilo lilikuwa na viongozi waliotetea mfumo wa ugatuzi wakati wa uhuru, ambao ulikuwa miongoni mwa sera za Bw Odinga,” akasema Prof Shauri.

Hata hivyo, alisema kuwa baada ya ujenzi wa SGR na wenyeji kuanza kulalamikia kupunguziwa nafasi za kazi na ujio wake, Bw Odinga alibaki kimya.

“Kimya cha Bw Odinga kilikuwa kama usaliti kwao kwani walianza kutia tashwishi yake kama mtetezi wa wanyonge. Hadi sasa, tatizo hilo bado halijapata suluhisho huku akiendelea kubaki kimya,” akaeleza mdadisi huyo.

Wadadisi wanaeleza uasi huo pia umechangiwa na uwepo wa kizazi kipya, kinachohisi kuwa ni wakati wao kuanza kujitetea wenyewe, kwani viongozi waliowategemea kama Bw Odinga wamefeli kufanya hivyo.

Kando na Bw Kingi na Bw Joho, magavana wengine wanaoshinikiza kubuniwa kwa chama kimoja cha kisiasa cha eneo hilo ni Granton Samboja (Taita Taveta) na Salim Mvurya (Kwale).

“Mazingira ya kisiasa yamebadilika sana. Ikizingatiwa Bw Odinga amekuwa akipata uungwaji mkono karibu miaka 20, kumechipuka kizazi kipya ambacho kinataka kutwaa uongozi wa eneo hilo chenyewe badala ya kumtegemea ‘mkombozi’ kutoka nje,” akasema Prof Hassan Mwamkimako, ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa za ukanda huo.

Baadhi ya vyama vikuu vya kisiasa eneo hilo ni Chama cha Uzalendo (CCU), Shirikisho Party na Kaddu Asili.Muungano wa Wataalamu Pwani (CPF) ulisema unafanya kila juhudi kuunganisha vyama hivyo ili kuhakikisha ukanda huo umepata chama kimoja cha kisiasa.

Mwenyekiti wa muungano huo, Bw Emmanuel Nzai, alisema ana imani juhudi hizo zitazaa matunda.“Nina imani kwamba hatimaye, Wapwani watapata jukwaa ambalo watakuwa wakitumia kuwasilisha maslahi yao kitaifa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Malala na Echesa mafichoni wakisakwa na polisi kwa kuzua...

Simba wa Ford Kenya anguruma Kabuchai