Siasa

Raila, Ruto watofautiana kuhusu ubadilishaji matokeo

April 21st, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga Jumamosi walitofautiana kuhusu iwapo marehemu Jenerali Francis Ogolla ni miongoni mwa wale waliotaka kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 2022.

Akiongea katika uwanja wa michezo wa Ulinzi, Nairobi, wakati wa ibada ya kumuenzi Jenerali Ogolla, Rais Ruto alifichua kuwa marehemu alikubali kosa hilo wakati wa mkutano wa faragha aliofanya naye baada ya kuingia afisini.

“Wakati ulipojiri wa kuteua mkuu mpya wa majeshi, mapendekezo na ushauri niliopata kuhusu yule niliyefaa kuteua hayakujumuisha jina la Jenerali Ogolla. Lakini alikuwa afisa wa jeshi mwenye tajriba kubwa na aliyehitimu kwa cheo hicho,” akasema Rais Ruto.

“Shida ya pekee niliyokuwa nayo ni matukio katika ukumbi wa Bomas mnamo Agosti 15, 2022. Niliomba kufanya mkutano wa ana kwa ana, wa kuja kwa Yesu naye. Tulipomaliza alisema ‘Siwezi kujitetea. Kilichotendeka kilikuwa kosa na una maamuzi matatu ambayo ni kunifungulia mashtaka katika mahakama ya jeshi, kunistaafisha mapema au kunisamehe’,” Rais Ruto akasema.

Kiongozi wa taifa ambaye pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote nchini, alisema kuwa hatimaye aliamua kumteua Ogolla sio kwa misingi ya kikabila bali uhitimu.

“Baada ya kutafakari kwa kina kuhusu yule niliyefaa kuteua kuwa Mkuu wa Majeshi, nilijikumbusha yaliyonipata katika mahakama ya ICC na kuamua kwamba tunapaswa kukumbatia mtindo tofauti kama nchi. Niliamua kuwa Jenerali Ogolla alipaswa kuwa Mkuu wa Majeshi. Ni uteuzi ambao nauonea fahari,” Rais Ruto akasema huku akimimina sifa kwa marehemu.

Bw Odinga ndiye alikuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo alipohutubu awali.

Akaeleza: “Jenerali Ogolla hakufika katika Bomas of Kenya kumlazimisha  Chebukati (aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC) kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais. Ninamjua alikuwa mwanajeshi aliyezingatia kazi yake. Tunataka hili suala likamilishwe tunapoomba Mungu aipumzishe roho yake pema.”

Rais Ruto na Bw Odinga walikuwa wakirejelea madai yaliyotolewa na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC mnamo Agosti 15, 2022, kwamba Jenerali Ogolla, wakati huo akiwa Naibu Mkuu wa Majeshi, alishirikiana na wengine kujaribu kumlazimisha kumtawaza Bw Odinga mshindi.

Katika hatikiapo iliyowasilishwa mahakamani wakati wa kesi ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto, Bw Chebukati pia alisema Ogolla na wengine vilevile walimtaka kuamuru marudio ya uchaguzi wa urais.

Bw Chebukati alidai kuwa Jenerali Ogolla aliandamana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, miongoni mwa maafisa wengine katika serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Jumamosi, Bw Odinga pia aliitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali ya ndege iliyosababisha kifo cha Jenerali Ogolla na maafisa wengine saba wa kijeshi.

“Uvumi umekuwa ukienea baada ya ajali hii iliyosababisha kifo cha Ogolla. Naomba serikali ifanye uchunguzi wa kina na chanzo chake kibainike wazi. Vilevile, ndege za idara ya ulinzi na vikosi vingine vya usalama zinafaa kugauliwa upya kuhakikisha kuwa ni salama kwa matumizi,” akasema.

Viongozi wengine wakuu waliohutubu katika hafla hiyo ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Waziri wa Ulinzi Aden Duale.

Jenerali Ogolla anazikwa Jumapili nyumbani kwake katika eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.