Raila sasa akimbilia mahakama

Raila sasa akimbilia mahakama

NA BENSON MATHEKA

MWANIAJI urais kwa tikiti ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kwenye uchaguzi mkuu wa wiki jana, Raila Odinga, amepinga matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, Bw Wafula Chebukati.

Bw Odinga alitaja matokeo hayo kama yasiyo ya kikatiba na haramu, na akatangaza kuwa atatumia njia za kikatiba kuyapinga Mahakamani.

“Tunatangaza kuwa tunakataa matokeo haramu na yasiyo ya kikatiba ambayo Bw Chebukati alitangaza jana (mnamo Jumatatu),” Bw Odinga alisema.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kwamba, Bw Chebukati alijaribu kupindua uamuzi wa Wakenya na “hatutakubali mtu mmoja azue vurugu katika nchi yetu”.

Mnamo Jumatatu jioni, Bw Chebukati alimtangaza Naibu Rais William Ruto mshindi wa uchaguzi wa urais akisema, alipata kura 7,176,141, dhidi ya 6,942,930 za Bw Odinga aliyeibuka wa pili.

Hata hivyo Jumanne, Bw Odinga alikataa kutambua matokeo hayo akilaumu Bw Chebukati kwa kwenda kinyume na mchakato wa kujumuisha na kutangaza matokeo ya kura ya urais.

Bw Odinga aliyezungumza katika Kenyatta International Conference Center (KICC) Nairobi alisema kwamba, matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati sio sahihi kwa kuwa hayakuidhinishwa na makamishna wote wa IEBC.

“Tunasisitiza kuwa tunakataa kabisa matokeo ambayo yalitangazwa jana na Bw Chebukati kwa kuwa, sio uamuzi wa makamishna wote wa tume hiyo,” alisema Bw Odinga aliyeandamana na mgombea mwenza wake, Bi Martha Karua na kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka.

Bw Odinga alisema kwamba, hatua ya Bw Chebukati ya kutangaza matokeo peke yake inaweza kutumbukiza nchi kwenye machafuko.

Alisema Bw Chebukati alikiuka sheria kwa kutangaza matokeo bila kuhusisha makamishna wenzake.

“Sheria iko wazi kuhusu jukumu la mwenyekiti wa IEBC. Sheria ya IEBC haimruhusu mwenyekiti wa IEBC kufanya maamuzi bila kushirikisha makamishna wenzake na iwapo hawakubaliani, sheria inasema uamuzi uafikiwe kwa kupiga kura,” alisema.

Bw Odinga alidai kwamba, Bw Chebukati aliwaficha makamishna wa tume matokeo aliyotangaza hadi dakika ya mwisho, hatua iliyofanya wengi wao kujiondoa katika Bomas of Kenya wakipinga uamuzi wake.

“Chebukati angetumbukiza nchi kwenye hatari kama wafuasi wengi hawangekuwa na subira,” alisema na kuwataka wafuasi wake waendelee kudumisha amani.

“Hakuna anayepaswa kuchukua sheria mikononi. Tunahimiza amani kote nchini huku tukifuata njia za kikatiba kufuta uamuzi wa Bw Chebukati,” alisema Bw Odinga.

Alisema hayo dakika chache baada ya makamishna wanne wa IEBC waliojitenga na Bw Chebukati kusisitiza kuwa, hawatambui matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022.

Bw Odinga alisisitiza kuwa, hatambui Dkt Ruto kama rais mteule.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Mikakati ya kufufua kahawa sasa yaanza kuzaa matunda

ZARAA: Teknolojia ndio itaokoa kilimo nchini, afisa asema

T L