Habari Mseto

Raila sasa aongoza harambee kanisani

November 4th, 2020 2 min read

OSCAR KAKAI na ONYANGO K’ONYANGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga aliongoza mkutano wa kuchangisha pesa kanisani Jumanne, licha ya kuwa kwenye mstari wa mbele kukosoa shughuli kama hizo zinapoendeshwa na Naibu Rais William Ruto.

Bw Odinga aliongoza harambee hiyo kusaidia Kanisa la Dini ya Mafuta Pole Africa lililoko eneo la Sook, Kaunti ya Pokot Magharibi ambapo alitumia jukwaa hilo kupigia debe marekebisho ya Katiba kupitia mapendekezo kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI).

Huku akionekana kumshambulia Dkt Ruto na washirika wake, Waziri huyo Mkuu wa zamani aliwakashifu wale wanaopinga mabadiliko ya Katiba kupitia BBI, akisema mpango huo unalenga kuchochea maendeleo nchini na kupunguza viwango vya umasikini.

“Tumetoka Misri, Bahari ya Shamu, Sinai na tulipofika mto Jordan tukapata mamba lakini tumeamua kuruka. Miaka 57 baada ya kupata uhuru tunataka kutimiza ndoto za mababu zetu kupelekea Kenya mbele. Kuna ukosefu wa ajira, umasikini na miundo msingi mbaya, changamoto ambayo tunapaswa kushughulikia sasa,” akasema.

Bw Odinga alikuwa ameandama na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, kiongozi wa wengi katika seneti Samuel Poghisio, Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi Profesa John Lonyangapuo, Mbunge wa Tiaty William Kamket, miongoni mwa viongozi wengine.

Kiongozi huyo wa ODM amekuwa akikosoa Dkt Ruto kutokana na mienendo yake ya kutoa fedha nyingi kanisani, akisema Naibu huyo wa Rais hutumia makanisa “kutakasa” pesa alizopata kwa njia za ufisadi.

Jumanne, Bw Odinga alisema ripoti ya BBI inapiga jeki ugatuzi kwa kupendekeza kuwa serikali za kaunti ziongezewe mgao wa fedha kutoka asilimia 15 hadi asilimia 35 ya mapato ya kitaifa.

“Kaunti nyingi zimeshindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu kiasi kikubwa cha fedha hutumika kulipia mishahara. Sasa kupitia BBI kaunti zitapokea kiasi kisichopungua asilimia 35 ya mapato ya serikali ambapo asilimia 5 zitatengewa maendeleo katika wadi ili kusawazisha maendeleo,” akaeleza.

Kwa upande wake, Profesa Lonyangapuo alisema viongozi wote wa Kaunti ya Pokot Magharibi wataunga mkono ripoti ya BBI.