Habari MsetoSiasa

Raila sasa ataka mbunge wa Westlands kuwa gavana wa Nairobi 2022

December 13th, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga amemuidhinisha mbunge wa Westlands, Bw Tim Wanyonyi kuwa gavana wa tatu wa Kaunti ya Nairobi.

Hatua ya Bw Odinga inatarajiwa kuzua mjadala wakati huu ambao siasa za 2022 zimepamba moto Nairobi.

Gavana wa kwanza wa Nairobi alikuwa Dkt Evans Kidero wa chama cha ODM ambaye alishindw na Mike Sonko wa Jubilee kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akiongea katika chuo cha ufundi cha Kabete alipohudhuria mechi ya soka iliyofadhiliwa na Bw Wanyonyi, Bw Odinga alisema mbunge huyo atapeperusha bendera ya ODM katika kura ya kiti cha ugavana.

“Ingawa niko hapa kama mchezaji na sio mwanasiasa,ninataka kusema gavana wa Nairobi atakuwa Tim. Anafanya kazi nzuri na anastahili tiketi ya ODM kwenye uchaguzi mkuu wa 2022,” alisema Bw Odinga.

Alisema rekodi ya maendeleo ya mbunge huyo ni nzuri na ndiyo ilimfanya ahudhurie mechi hiyo ili kumuunga mkono.

Bw Odinga alisema kiwango cha soka nchini kinaimarika kufuatia kufuzu kwa timu ya taifa Harambee Stars kucheza katika fainali ya mataifa bingwa barani Afrika

Bw Wanyonyi pia aliungwa mkono na viongozi wengine wa ODM waliohudhuria mechi hiyo.

Wabunge Babu Owino, George Aladwa, Antony Oluoch na madiwani kadhaa walihudhuria hafla hiyo.