Raila sasa tayari kukubali reggae ikizimwa kabisa

Raila sasa tayari kukubali reggae ikizimwa kabisa

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ametangaza kuwa atakubali uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu hatima ya mchakato wa mageuzi ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) utakaotolewa kesho.

Akiongea Jumanne wakati wa ziara yake mjini Nakuru, Bw Odinga hata hivyo alikariri kuwa hata kama jopo la majaji saba wa mahakama hiyo litazima mpango huo wa marekebisho ya Katiba hiyo haitakuwa mwisho wa ndoto hiyo.

“Tutasubiri uamuzi wa mahakama. Ikiwa wataamua vizuri ni sawa na ikiwa wataamua kinyume cha matarajio yetu, mimi na rais Kenyatta hatutaelekea katika Mahakama ya Juu,” Bw Odinga akaambia umati wa watu katikati mwa barabara ya Kenyatta Avenue, mjini Nakuru.

Bw Odinga alirudia kauli hiyo jana katika mahojiano na Redio Nam Lolwe, kwa njia ya simu.Katika ziara yake mjini Nakuru, waziri huyo mkuu wa zamani alitangaza kuwa hivi karibuni atatangaza muungano ambao utaunganisha Wakenya kutoka pembe zote za nchini.

‘Hivi karibuni tutazindua chombo ambacho kitawaunganisha Wakenya wote na kuwapeleka katika nchi ya ahadi. Sharti tutoe suluhu la shida zinazoisibu nchini hii katika nyanja zote za uchumi na siasa,’ akaeleza.

Bw Odinga alikuwa ameandamana mwenyeji wake, Gavana Lee Kinyanjui na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya. Wengine waliokuwepo ni; Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na wabunge Junet Mohammed (Suna Mashariki), Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Maina Kamanda (Mbunge Maalamu) miongoni mwa wanasiasa wengine.

Jopo la Majaji saba wa Mahakama ya Rufaa chini ya uongozi wa rais wake, Daniel Musinga, wanatarajiwa kuamua ikiwa watakubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuharamisha mchakato huo au la.

Katika uamuzi wake wa mwezi Mei 13 mwaka huu, jopo la majaji watano wa Mahakama Kuu waliamua kuwa, mswada wa marekebisho ya katiba ulikiuka Katiba kwa sababu umma haukushirikishwa inavyopaswa.

Majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Teresia Matheka na Chacha Mwita pia walikosoa hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kutumia mamlaka ya afisi yake na fedha za umma kuanzisha na kuendesha mchakato huo.

Mwezi jana, Bw Odinga alisema yeye na Rais Kenyatta wako na njia mbadala ya kufanikisha mageuzi ya Katiba endapo mahakama ya rufaa itazima mageuzi yanayopendekezwa kupitia mpango wa BBI.

Mwezi jana akiongea katika redio Citizen kiongozi huyo wa ODM akasema: “Endapo mahakama itafutiliwa mbali BBI, tuko na mkondo mbadala wa kufanikisha mageuzi ya katiba.”

Wakereketwa wa BBI wakiongozwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga waliwasilisha kesi katika mahakama ya rufaa, wakitaka ibatilishe uamuzi wa Mahakama kuu ulizima mpango huo wa marekebisho ya katiba.

Kwa mfano, mawakili wa Rais Kenyatta waliambia jopo hilo la Jaji Musinga kwamba kiongozi wa taifa pia yuko na uhuru wa kuanzisha mchakato wa mageuzi ya katiba.

“Kwanza kabisa Rais Kenyatta ni raia wa Kenya kabla ya kuwa na wadhifa huo,” akasema Mkuu wa Sheria wa zamani Profesa Githu Muigai aliyeongoza mawakili wa rais katika kesi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Amerika yafungia Taliban pesa

BENSON MATHEKA: Viongozi waungane, ndio, lakini wasigawanye...