Raila: Sehemu muhimu za chanjo ni sokoni, shuleni

Raila: Sehemu muhimu za chanjo ni sokoni, shuleni

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa ODM Bw Raila Odinga ameihimiza serikali kulenga maeneo yenye idadi ya juu ya watu katika operesheni yake ya utoaji wa chanjo ya virusi vya corona.

Amesema maeneo ya umma kama vile shule na masoko yakipewa nafasi ya mbele, Kenya itafanikisha vita dhidi ya janga la Covid-19.

Alisema mataifa kama vile Amerika na Uingereza, yameweza kufungua chumi zao kikamilifu kwa kulenga makundi ya watu wanaotoa huduma za umma, katika mchakato mzima wa utoaji uchanjo.

“Ni vizuri tuangalie vile nchi nyingine kama vile Amerika na Uingereza zimefanya katika utoaji wa chanjo,” akasema.

“Kule Uingereza wamefungua uchumi kikamilifu kwa sababu watu walio na zaidi ya umri wa miaka 30 wote wamepata chanjo. Mambo ya maski hawana. Hilo linawezekana huku kwetu. Tutii agizo la serikali watu wapate chanjo,” akaongeza.

Akitumia mfano wa enzi za ukoloni, kinara huyu wa ODM alisema mlipuko wa magonjwa ibuka ulikabiliwa kupitia utoaji chanjo zaidi katika shule na masoko.

“Ninakumbuka ukambi ulipochipuka, chanjo ilitolewa kwa wingi kwa wanafunzi na wahudumu wa masoko. Chini ya mwaka mmoja, kila mtu nchini alikuwa amepata chanjo,” akaelezea.

Ameyasema hayo Ijumaa kupitia mahojiano ya moja kwa moja na runinga ya Inooro, inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

Aidha, alihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo.

“Watu wasikubali hadaa kuwa chanjo inayotolewa ina athari. Hizo ni projo ambazo ni potovu tu,” akasema.

Serikali inalenga kutoa chanjo kwa watu milioni 10 kufikia Desemba 2021.

You can share this post!

Mendy asimamishwa kazi na Man-City kwa hatia ya ubakaji

Wafanyakazi 9 wafa kwa kuanguka na kreni