Habari za Kaunti

Rais aahidi kufanya Homa Bay kuwa jiji


HOMA BAY huenda ikapandishwa hadhi na kuwa jiji jipya hivi karibuni kufuatia ahadi iliyotolewa na Rais William Ruto Alhamisi.

Iwapo ahadi ya Kiongozi wa Taifa itatimia, Homa Bay itajiunga na orodha ya majiji matano ya humu nchini yanayojumuisha Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret, iliyotwikwa majuzi hadhi ya jiji.

Akizungumza Alhamisi wakati wa ziara yake eneo hilo, Rais Ruto aliahidi kufanya mji wa Homa Bay kuwa moja kati ya majiji nchini, akisema serikali yake imejitolea kuinua eneo hilo.

Japo hakusema ni lini ahadi hiyo itatekelezwa, alitangaza baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo serikali yake inaendesha ili kuhakikisha mji huo unakua.

“Tunapanga kufanya Homa Bay iwe mji na nitahakikisha hilo limefanyika,” alisema Dkt Ruto Alhamisi.

Hadhi ya jiji 

Ili eneo lipandishwe hadhi kuwa jiji, Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi na Mahusiano ya Serikali za kaunti inahitajika kutoa idhini.

Sheria iliyofanyiwa marekebisho kuhusu Maeneo ya Mijini na Majiji 2019 kuhusu kuorodhesha mji kuwa jiji, inasema eneo la mji husika ni sharti liwe na idadi ya watu wasiopungua 250,000.

Idadi hii inafaa kuendana na matokeo ya mwisho yaliyochapishwa kwenye notisi rasmi kuhusu shughuli ya kuhesabu watu.

Aidha, mji husika unahitajika kuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu kwa wakazi wake na ni sharti uwashirikishe wakazi wake mara kwa mara katika usimamizi wa masuala yake.

Matakwa mengine ni pamoja na kuwa na miundomsingi bora ikiwemo barabara, taa za barabarani, masoko, mfumo thabiti wa kuzoa taka na kupatia kipaumbele mbinu za kukabiliana na majanga.

Homa Bay, hata hivyo, bado haijatimiza baadhi ya masharti hayo.

Gavana Gladys Wanga aliyempokea Rais alisema usimamizi wake utafanya Homa Bay kuwa jiji katika muda wa miaka 10.

Alisema anataka kuweka historia kuwa gavana aliyeongoza Homa Bay kuinuka katika viwango vipya.

Serikali ya kaunti hiyo inatumia mpango wenye thamani ya mamilioni unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa lengo la kuinua makazi ya vitongoji duni.

Hii ni kupitia kuzibua mifereji ya majitaka, kuweka taa za barabarani na kuboresha miundomsingi ya masoko.

Dkt Ruto amesema utawala wake umejitolea kuboresha sekta kuu za kiuchumi ili kuwezesha maendeleo Homa Bay.

Maendeleo hayo yanajumuisha kusambaza umeme, maji, barabara, biashara na kukamilisha uwanja wa spoti wa Raila Odinga.

Katika ziara yake, Rais alikagua ujenzi unaoendelea wa soko la samaki la Homabay lenye nafasi ya wafanyabiashara wasiopungua 400.

Aligiza mradi huo ukamilishwe kufikia Disemba atakaporejea kuwafungulia rasmi wafanyabiashara kuanza kutumia soko hilo jipya.

Alisema serikali yake imetenga Sh600 milioni za kuboresha mfumo wa barabara mjini Homa Bay.

Kulingana na Rais, ameafikiana na serikali ya kaunti hiyo kutenga Sh1.5 bilioni za mradi wa kusambaza umeme kwa watu wasiopungua 17,000.