Rais aenda mteja raia wakiumia

Rais aenda mteja raia wakiumia

Na SAMMY WAWERU

SAA chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza ‘lockdown’ katika kaunti tano na kurefusha muda wa kafyu mnamo Machi 26, trakta za ubomoaji zikilindwa na polisi zilivamia mtaa wa Ruai, Nairobi.

Baada ya muda mfupi, makao ya watu wapatao 5,000 yalikuwa yamebomolewa.

“Tuliamshwa saa tisa alfajiri, matingatinga yalipofika na kuanza kubomoa nyumba zetu huku polisi wakiturushia gesi ya vitoa machozi. Hakuna nilichookoa isipokuwa mtoto na nguo tulizokuwa tumevaa. Nilikuwa chuoni kimaisha lakini serikali imenirudisha nasari,” Jacinta Wanjiku, 25, anasimulia machozi yakimdodoka machoni.

Saa chache kabla ya maisha ya wakazi hao 5,000 kuharibiwa, tayari ya maelfu ya wakazi wa Nairobi, Nakuru, Machakos, Kajiado na Kiambu yalikuwa yamesambaratishwa kwa agizo la Rais Kenyatta la kufungwa kwa mikahawa, mabaa na kusitishwa kwa usafiri kutoka Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru.

Wamiliki wa biashara hizo na magari pamoja na wafanyikazi wao waliachwa jangwani bila chakula wala maji.

Rais Kenyatta hakuonyesha kuwajali waathiriwa hao hata kidogo alipohepa kutangaza hatua yoyote ambayo serikali ingechukua kuwapa afueni kimaisha.

Mbali na maelfu kupoteza ajira, wakazi wengine wa kaunti hizo nao waifinyika kwa kafyu inayoanza saa mbili, kwani inabidi wafunge biashara zao mapema ili kuwa nyumbani wakati ufaao.

Kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea jijini Nairobi pamoja na mfumo duni wa uchukuzi wa umma, ambao serikali imeshindwa kuboresha, misongamano ya watu na magari jioni imekuwa kawaida.

Bila kujali uhalisia wa mambo haya, mnamo Jumamosi iliyopita serikali ilianza kutumia nguvu kupindukia dhidi ya raia, wengi wao wakiwa wanatoka kazini.

Barabara zinafungwa saa mbili, hali inayofanya wagonjwa kushindwa kufika hospitalini na watoaji huduma muhimu kulemewa kusafiri.

Mnamo Jumatatu, wanafunzi wa kidato cha nne waliokuwa wamemaliza mtihani wao walilazimika kulala katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi baada ya kushindwa kufika makwao kutokana na kafyu.

Matukio haya ya serikali kuwadhulumu raia, yanazua maswali kuhusu iwapo kama kweli nia yake ni kupunguza maambukizi ya corona ama kuna njama fiche ya kukadamiza wananchi kwa lengo fulani la kisiasa.

“Yanayoendelea ni kuwepo kwa hali ya hatari kwa visingizo vya kukabiliana na Covid-19. Hii ni mbinu ya utawala wa kimabavu kuchukua fursa ya janga la kiafya kuwahujumu raia,” asema Mkurugenzi Mkuu wa International Centre for Policy and Conflict, Ndung’u Wainaina.

“Hatua ambazo Rais Kenyatta ametangaza zinapuuza ukweli kuwa Wakenya wengi wanategemea uchukuzi wa umma ambao umeoza, pamoja na ajira ya kubahatisha. Wakenya wa kawaida wamenyanyaswa, kuaibishwa na kunyamazishwa,” akaongeza Bw Wainaina.

MATESO TUPU

“Haya ni mateso tupu kwa sababu serikali imeamuru kafyu ianze mapema ilhali tunapasa kutoka kazini kawaida. Mimi hufanya kazi Westlands na ninaishi mtaa wa Pipeline. Nalazimika kuchelewa kufika nyumbani kila siku kutokana na foleni ndefu katika kituo cha matatu,” asema Bi Judith Oloo.

“Ninafanya kazi Upperhill na naishi Utawala. Natoka kazi saa kumi na moja jioni, natembea hadi kati mwa jiji kuchukua matatu ambayo kawaida ninaabiri saa moja. Kisha natumia masaa mawili katika barabara ya Mombasa Road, hivyo lazima nichelewe kufika nyumbani,” asema mkazi mwingine.

Kwa upande Bw John Irungu, mkazi wa eneo la Banana, Kiambu alielezea hofu ya kuambukizwa corona ikiwa serikali haitapunguza muda wa kafyu.

“Hii kafyu ya kuanzia saa mbili usiku haitapunguza visa vya maambukizi ya corona kwa sababu matatu hujaza watu kupita kiasa kwa sababu kila mtu anataka kufika nyumbani,” akasema Bw Irungu.

Wataalamu wa afya wanasema kufungwa kwa kaunti tano na kuongezwa kwa muda kafyu kulifaa kuambatana na shughuli mahsusi zaa chanjo na kuwapima wakazi wa kaunti hizo.

“Hali hii ni hatari zaidi kwani serikali ilifaa kufunga kaunti hizi tano kisha ianzishe mchakato wa upimaji corona na utoaji chanjo. Ilivyo sasa ni kwamba huenda hatua ya kufungwa kwa kaunti hizo na muda wa kafyu kuongeza kusilete faida,” asema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Lancet Kenya, Dkt Ahmed Kalebi.

  • Tags

You can share this post!

‘Nahisi upweke licha ya kuwa kwenye ndoa’

Jubilee kuvunja uhusiano na PDR ambacho sasa ni UDA