Rais ahimiza Wakenya kujiandikisha kwa bima ya afya ya NHIF, akizindua rasmi mpango wa UHC

Rais ahimiza Wakenya kujiandikisha kwa bima ya afya ya NHIF, akizindua rasmi mpango wa UHC

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kujiandikisha kwa bima ya afya ya NHIF ili kupunguza gharama ya matibabu.

Kiongozi huyo wa nchi alisema gharama ya matibabu na ambayo inaendelea kulemea Wakenya wengi itapungua endapo kila mwananchi atachukua kadi ya NHIF. Alisema hayo katika eneo la Changamwe, Mombasa, wakati akizindua rasmi Mpango wa Afya Kwa Wote, UHC.

“Safari ya Mpango wa Afya kwa Wote, tumeitembea kwa muda mrefu, lililosalia sasa ni Wakenya wachukue kadi ya NHIF,” Rais akahimiza. Mpango wa UHC, na ambao unalenga kutoa afya bora kwa wote na kwa bei nafuu ulifanyiwa jaribio katika kaunti nne 2018.

Mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Rais Kenyatta baada ya kuchaguliwa 2017 kuhudumu awamu yake ya pili na ya mwisho, ni kuhakikisha kila Mkenya anapata afya bora na nafuu. Huku ghamara ya matibabu ikizidi kulemea wengi, Rais Kenyatta amesema kila mwananchi kuwa na bima ya afya ni kati ya mbinu kukabiliana na umaskini.

“Kama Wakenya tunataka kumaliza ufukara, hatutaumaliza ikiwa unaingia kwako bila kadi ya NHIF ugonjwa ukibisha hodi unatumia maelfu ya pesa kuutibu,” akasisitiza. “Tunataka mambo ya magonjwa kufilisisha mtu yaishe nchini mwetu. Wakenya wenzangu tuchukue na kujiandikisha kadi ya NHIF, tujiokoe kiafya na kihela,” Rais akahamiza.

Akitumia mfano wa maradhi ya Saratani, Rais Kenyatta alieleza kusikitishwa kwake na gharama ya juu ambayo hutumika kukabili makali. Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ya Rufaa na Mafunzo (KU Referral) na ile ya Rufaa ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), ni kati ya zinazotoa huduma za matibabu ya Kansa.

Chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya KU Referral, Prof. Olive Mugenda, Rais Kenyatta amepongeza hospitali hiyo kufuatia mchango wake mkuu. “Kufikia sasa, imeweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 200 wa Saratani. Hii ni ishara kuwa kama taifa tunapiga hatua mbele kuboresha huduma za matibabu,” akadokeza.

Rais aidha alisema baadhi ya hospitali za umma zinapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi, hatua aliyosema serikali yake inaridhia kutokana na mikakati maalum aliyoweka kuimarisha sekta ya afya. “Hivi karibuni gharama ya matibabu katika hospitali za serikali itashuka, na vituo vya afya vya kibinafsi havitakuwa na budi ila kupunguza malipo,” akasema.

You can share this post!

Messi aongoza PSG kuponda Lille na kufungua mwanya wa alama...

Soyaux-Charente anayochezea Mkenya Awuor yazoa ushindi Ligi...

T L