Habari Mseto

Rais akagua miradi ya nyumba Nairobi

May 22nd, 2019 1 min read

PSCU Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alifanya ziara ya ghafla kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba na barabara Jijini Nairobi.

Rais alizuru mtaa wa Parkroad ulioko Ngara ambako serikali inajenga nyumba 1,370 huku awamu ya kwanza ya nyumba 228 zikitarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Mradi huo wa ujenzi wa nyumba ni mojawapo wa mpango wa Serikali wa kujenga nyumba 500,000 za bei nafuu ifikapo mwaka wa 2022 chini ya nguzo ya ujenzi wa nyumba ya Ajenda Kuu 4 Kuu za Maendeleo.

Rais ambaye alikuwa ameandamana na Waziri wa Uchukuzi na Muundo Msingi James Macharia na mwenzake wa Fedha Henry Rotich alimhimiza mwanakandarasi wa mradi huo kuhakikisha viwango bora vinazingatiwa.

Alisema mradi huo ni wa majaribio ambao utatumika kama kielelezo cha ujenzi wa nyumba za aina hiyo katika miji yote nchini.

“Mradi huu utatumika kama mfano kwa miradi mingine ambayo itatekelezwa katika miji mingine kama vile Mombasa, Kisumu, Eldoret,” akasema Rais Kenyatta.

Mapema, Rais alikagua ujenzi unaoendelea wa barabara ya kuunganisha barabara ya Waiyaki hadi Red Hill.

Bw Macharia alimuongoza Rais katika ziara hiyo na kumuarifu kuhusu ujenzi unaoendelea wa barabara nyingine ikiwemo awamu ya pili ya barabara ya safu mbili ya Ngong.

Akiwahutubia wafanyakazi katika mradi wa ujenzi wa nyumba, Rais Kenyatta aliwahimiza wahakikishe wamejisajili kwa Huduma Namba.

Rais Kenyatta aliwaagiza maafisa wa utawaka kaunti ya Nairobi kuhakikisha maafisa wa usajili wanapelekwa katika maeneo ya mijengo mnamo siku ya Alhamisi kuhakikisha wafanyakazi wa mijengo wanasajiliwa.