Habari MsetoSiasa

Rais akejeliwa kwa kuzomea viongozi

June 18th, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

VIONGOZI katika eneo la Mlima Kenya, wamemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kutumia hafla ya kidini mnamo Jumapili kuwazomea baadhi ya wanasiasa wanaoendeleza siasa za urithi wa 2022.

Mnamo Jumapili akiwa katika mkutano wa Wakorino, Rais Kenyatta, ambaye alikuwa na hasira nyingi, alitumia maneno makali ya matusi dhidi ya wanasiasa ambao alisema wanatumia muda wao mwingi kupiga siasa badala ya kuhudumia wananchi.

Hapo Jumatatu, Askofu Peter Mburu wa Muungano wa Dini za Kiasili (KICU) alisema Rais Kenyatta alivuka mipaka kwa kutumia shughuli ya kidini kutusi wengine.

“Matamshi ya Rais hayana tofauti na yale ambayo yamekuwa yakijadiliwa ya Kasisi James Ng’ang’a wa kanisa la Neno,” akasema Askofu Mburu.

Hii ni kuhusu kanda ya video ambapo Kasisi Ng’ang’a alinaswa akiwatusi maaskofu wa dhehebu lake.

“Hasira, maneno chafu na matusi hayafai kupewa nafasi kanisani na hafla za kidini,” Askofu Mburu akasema,

“Rais alitumia lugha chafu kwa hasira, akasuta wengine kwa kuwadunisha, akawatusi na akawapa vitisho. Rais anapasa kuwa na subira na kujizuia,” akasema Askofu Mburu.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi pia aliunga mkono msimamo wa Askofu Mburu akisema hotuba ya Rais ingekuwa na uzito mwingi ikiwa angeepuka matusi.

Bw Kaguthi alisema Rais akiwa nembo ya umoja wa kitaifa ni kielelezo kwa wengi hasa watoto, na anafaa kujizuia kuonekana kama asiye na uwezo wa kuthibiti hisia zake hadharani.

Akizungumza jana asubuhi kuhusu matamshi ya Rais Kenyatta ambapo aliwataja wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kama “takataka”, Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria alisema kuna haja ya viongozi wa Mlima Kenya kukutana ili kuzima migawanyiko inayoibuka kutokana na siasa.

Bw Kuria alisema kisa cha wiki iliyopita ambapo Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Bi Sabina Chege alizomewa na wananchi ni ishara ya haja ya kutuliza siasa, na kuchukua msimamo wenye manufaa kwa wakazi wa eneo hilo