HabariSiasa

Rais alipitisha walowezi wahamishwe Mau – Oguna

September 5th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI imewazima wanasiasa wanaotetea wakazi walioagizwa kuhama msitu wa Mau, Kaunti ya Narok, ikisema hatua hiyo ilipitishwa na Baraza la Mawaziri na itatekelezwa kikamilifu ilivyopangwa.

Msemaji wa serikali, Kanali mstaafu Cyrus Oguna, Alhamisi alieleza kwamba serikali hailengi msitu wa Mau pekee bali wakazi wanaoishi katika misitu ya Mlima Kenya na Aberdare pia watahamishwa.

Kauli hii ililenga viongozi kutoka Rift Valley ambao wamekuwa wakiikosoa hatua ya serikali ya kuwafurusha wakazi kutoka msitu wa Mau wakimlaumu Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko kwa kutumia mamlaka yake vibaya.

Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen, alidai kwamba serikali haikuwa imetoa agizo la kufurusha wakazi kutoka Mau akisema Bw Tobiko alikuwa akitumiwa na watu wanaotaka kumzuia Naibu Rais kushinda urais kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Bw Murkomen aliongoza wanasiasa wengine kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kujitokeza na kueleza iwapo amempa Bw Tobiko agizo la kufurusha wakazi kutoka msitu huo.

Jana, Bw Oguna alisema wakazi hao watahamishwa sawa na wanaoishi katika misitu mingine nchini na hakuna njama fiche jinsi wanasiasa hao walivyodai.

Hata hivyo, alisema shughuli hiyo itafanywa kwa njia ya utu.

“Ufurushaji wa watu kutoka msitu wa Mau lazima utekelezwe ili kuokoa nchi yetu lakini hilo litafanywa kwa njia ya utu. Neno muafaka kutumia hapa ni kuhamisha familia hizo na sio kuzitimua,” alisema Bw Oguna akihutubia wanahabari katika kikao cha kila Alhamisi.

Alisisitiza kuwa serikali inaelewa changamoto zilizopo na italinda hadhi ya watu.

Serikali inalenga kuwaondoa wakazi wanaozidi 60,000 kutoka msitu wa Mau. Iliwapa makataa ya siku 60 kuondoka, makataa yatakayokamilika Oktoba 30 mwaka huu.

Tayari watu wameanza kuondoka katika msitu huo licha ya wanasiasa kuwataka kukaidi agizo la serikali.

Maeneo ambayo watu wamehama ni Sierra Leone, Enokishomi, Enoosokon, Nkaroni, Nkoben, Ilmotiok, Ololung’a na Sisian.

Wakazi hao walisema waliamua kuhama wakiogopa maafisa wa usalama ambao wametumwa eneo hilo.

Ripoti za Benson Matheka, Anita Chepkoech na George Sayagie