Rais apanga kuunda miungano ya amani

Rais apanga kuunda miungano ya amani

Na JUSTUS OCHIENG

RAIS Uhuru Kenyatta anapania kuunda miungano ya kisiasa itakayoleta umoja nchini kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Hii ni kutokana na mizozo inayoshuhudiwa katika serikali ya Jubilee kati ya wandani wake na wale wa naibu wake, Dkt William Ruto ambao sasa wanaegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Kupitia chama cha Jubilee, Rais Kenyatta anapanga kufanya kazi pamoja na vyama vingine vya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ili kukomesha ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika chaguzi zilizopita.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Jumapili, Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju alithibitisha kuwa Rais anataka kuhakikisha kuwa kuna utulivu nchini kabla ya kustaafu mwaka 2022.

Tayari Jubilee imetia saini mkataba wa muungano kati yake na chama cha Kanu na iko mbioni kutia saini mkataba kama huo na chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka na CCM chake Bw Isaac Ruto.

Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga pia amekuwa akishirikiana na Rais Kenyatta tangu wawili hao waliporidhiana kisiasa mnamo Machi 9, 2018 kupitia salamu ya heri maarufu kama handisheki.

“Sisi kama Jubilee tunataka miungano inayowaleta Wakenya pamoja. Miungano ambayo italeta amani na ufanisi kimaendeleo nchini,” Bw Tuju akasema.

“Hii ndiyo maana tumekuwa tukifanya mazungumzo na ODM, Wiper, Ford-Kenya, ANC, Kanu na vyama vingine. Hii ni kwa sababu kimsingi, sote tu Wakenya, dada na kaka tunaoishi katika taifa hili tulilorithi kutoka kwa mababu zetu,” akaongeza.

Lakini juzi, Bw Odinga alitofautiana na vinara wenzake katika Nasa; Bw Musyoka, Mudavadi, na kinara wa Ford-K, Bw Moses Wetang’ula. Hii ni baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kutangaza kuwa hataidhinisha yeyote kati ya watatu hao kwa kiti cha urais 2022.

Bw Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula sasa wameungana na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kubuni vuguvugu la One Kenya.

Hatua hii imelazimisha Bw Odinga kuanza harakati za kuunda muungano mwingine unaowashirikisha kiongozi wa Narc Charity Ngilu, kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap Dkt Alfred Mutua na magavana Hassan Joho (Mombasa), Wycliffe Oparanya (Kakamega), Kivutha Kibwana (Makueni) na waziri wa zamani Mukhisa Kituyi.

Hata hivyo, Bw Tuju anasema kuwa ushindani kati ya vinara hao wa zamani wa Nasa ni jambo la kawaida mradi usitumbukize taifa katika ghasia zilizoshuhudiwa nchini 2007.

“Bila kujali ikiwa tuko ndani ya ODM, Jubilee, UDA au vyama vingine, muhimu ni kwamba sote ni Wakenya. Hii ndio maana Rais anataka kuunganisha Wakenya wote,” akariri Katibu huyo Mkuu wa Jubilee.

You can share this post!

MALENGA WA WIKI: Ali Mtenzi, mshairi stadi anayetamba pia...

JAMVI: Athari ya Uhuru kusema ‘fulani’ tosha