Habari

Rais apendekeza majina ya watu watakaohudumu kama makamishna NCIC

October 23rd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alimpendekeza Kasisi Samuel Kobia kuwa mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC).

Vilevile, kiongozi wa taifa aliwapendekeza watu wafuatao kuwa wanachama wa tume hiyo.

Wao ni: aliyekuwa mbunge wa Rangwe Philip Okundi, Samuel Kona, Peris Nyutu, aliyekuwa Mbunge wa Mandera Abdulaziz Ali Farah, aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Kaunti ya Nairobi Danvas Makori, Fatuma Tabwara na aliyekwua Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Vihiga Dorcas Kedogo.

Majina hayo sasa yatawasilishwa kwa Bunge la Kitaifa ili yapigwe msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Uwiano na Usawa inayoongozwa na Mbunge Maalumu Maina Kamanda.

Ikiwa uteuzi wao utaidhinishwa, watu hao watachukua pahala pa makamishna walioongozwa na Spika wa zamani Francis Ole Kaparo ambao muda wao wa kuhudumu ulikamilika Septemba 2018.

Kasisi Kobia alizaliwa mwaka 1947.

Yeye ni Kasisi wa Kanisa la Kimethodisti na Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) ambako alihudumu kati ya miaka ya 2004 hadi 2009.

Ajiuzulu

Kasisi Kobia pia alihudumu kama Kamishna katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kati ya miaka ya 2013 na 2015, kabla ya kujiuzulu ghafla.

Januari 2019, Mahakama Kuu iliamua kuwa shughuli ya uteuzi wa makamishna katika tume ya NCIC kupitia bunge ilikuwa kwenda kinyume cha Katiba.

Mahakama ilisema kuwa uteuzi wowote ambao utapitia bunge itachukuliwa kuwa batili.

Jaji Wilfrida Okwany alisema, katika uamuzi wake, kwamba Bunge la Kitaifa halina mamlaka ya kuendesha uteuzi wa watu kuhudumu katika tume hiyo.

Awali, Kamati ya Bunge kuhusu Uwiano na Usawa ilikuwa imeanza shughuli ya kuteua watu saba ambao walifaa kushikilia nyadhifa za makamishna wa tume hiyo.

Ilikuwa inapanga kuwahoji watu 54 waliokuwa wameorodheshwa kutoka kwa zaidi ya watu 200 waliotuma maombi.

Mahojiano hayo yangefanyika Novemba 12 hadi Novemba 14.